Breaking🔥

KAMATI YA UCHUMI, UJENZI NA MAZINGIRA YAIBUA CHANGAMOTO ZA MAENDELEO LONGIDO

KAMATI YA UCHUMI, UJENZI NA MAZINGIRA YAIBUA CHANGAMOTO ZA MAENDELEO LONGIDO

Na Joseph Ngilisho |LONGIDO.

KAMATI ya Kudumu ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira ya Halmashauri ya Wilaya ya Longido imeitaka Halmashauri kuchukua hatua za haraka kukabiliana na changamoto za miundombinu, mazingira, uwekezaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika wilaya hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ndiono Nangeresa, wakati akiwasilisha taarifa ya Kamati katika Baraza la Madiwani, kikao cha tano cha robo ya nne ya mwaka.

Nangeresa amesema Kamati imebaini kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazohitaji ushirikiano kati ya Halmashauri, viongozi wa Wilaya, wananchi na wadau wa maendeleo ili kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza kasi ya maendeleo.

Amesema miongoni mwa changamoto zilizobainika ni upungufu wa watumishi katika baadhi ya sekta, wakiwemo maafisa ugani, wataalamu wa mifugo, maafisa utalii na maafisa afya, hali inayoweza kuathiri utekelezaji wa majukumu ya Halmashauri.

Kamati imeishauri Halmashauri kuendelea kutenga fedha katika bajeti za kila mwaka kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya watumishi kwa mujibu wa ikama.

Aidha, amesema kuna upungufu wa miundombinu ya mifugo, hususan mabwawa ya kunyweshea mifugo, ambayo baadhi yake huharibiwa na mvua na kujaa matope.

Kwa mujibu wa Nangeresa, Halmashauri imeendelea kutenga fedha katika bajeti ya mwaka 2026/2027 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu hiyo, huku ikishirikiana na wadau kupata fedha za kuongeza huduma hizo.

Katika eneo la miradi ya maendeleo, Kamati imeeleza kuwa ufinyu wa bajeti umechangia kuwepo kwa miradi ya viporo, hivyo kuishauri Halmashauri kuendelea kuelekeza mapato ya ndani katika miradi hiyo na kuweka mikakati ya kuikamilisha kwa awamu.

Kamati pia imeonya kuhusu baadhi ya wafanyabiashara kutokuzingatia matakwa ya kisheria katika uendeshaji wa biashara zao, na kuishauri Halmashauri kuendelea kutoa elimu pamoja na kuchukua hatua kwa wanaokiuka sheria na taratibu za biashara.

Katika suala la mazingira, Kamati imebainisha ongezeko la uchafu katika maeneo ya Namanga, Longido na Orbomba, likisema hali hiyo inaweza kuhatarisha afya za wananchi, mazingira na miundombinu ya miji, ikiwemo kuziba kwa mitaro ya maji.

Nangeresa amesema Kamati imependekeza Halmashauri kutoa kipaumbele katika bajeti ya mwaka 2026/2027 kwa ajili ya kuboresha huduma za uendeshaji wa dampo na usafi wa mazingira, huku viongozi wa Wilaya na wadau wakitakiwa kufuatilia upatikanaji wa fedha zilizotengwa na TARURA kwa ajili ya barabara ya Kimokwawa–Dampo.

Katika eneo la uwekezaji, Kamati imependekeza Halmashauri kushirikiana na wanahisa wa Longido North Company Limited kutafuta mtaji utakaowezesha kampuni hiyo kutekeleza majukumu yake na kuongeza manufaa kwa wananchi na Halmashauri.

Pia, Kamati imetaka kufuatiliwa kwa karibu utekelezaji wa mkataba kati ya Vijiji vya Orbomba na Kimokwawa na Kimokwawa Aggregate Limited, ili kuhakikisha vijiji na Halmashauri vinapata mapato yanayotokana na uzalishaji wa kokoto kwa mujibu wa makubaliano.

Kuhusu utalii na uhifadhi, Kamati imeitaka Halmashauri kwa kushirikiana na viongozi wa Wilaya kufuatilia utekelezaji wa masharti ya mkataba wa Green Mine Safari Limited, ikiwemo kuhakikisha kampuni hiyo inashiriki ipasavyo katika shughuli za maendeleo ya jamii katika maeneo yanayohusiana na kitalu chake.

Wakati huo huo, Kamati imependekeza hatua zaidi zichukuliwe kudhibiti mbwa wanaozurura hovyo na wasiochanjwa, kutokana na matukio ya kushambulia na kuua mifugo.

Aidha, imependekeza wakulima waliosajiliwa katika mfumo wa ruzuku ya mbolea na mbegu kupewa elimu kuwa wanaweza kuchukua pembejeo hizo katika vituo vilivyoidhinishwa nchini ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa pembejeo katika Wilaya ya Longido.

Katika suala la wanyamapori, Kamati imebainisha kuwepo kwa matukio ya tembo kuharibu mashamba ya wananchi, huku ikishauri wataalamu wa wanyamapori na maafisa ugani kuendelea kutoa elimu kwa jamii na kuweka mikakati ya kupunguza migogoro kati ya wananchi na wanyamapori.

Nangeresa amesema utekelezaji wa mapendekezo hayo unalenga kuongeza ufanisi wa Halmashauri, kuboresha huduma kwa wananchi, kulinda mazingira na kuhakikisha rasilimali za Wilaya ya Longido zinawanufaisha wananchi na Serikali kwa ujumla.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم