POLISI ARUSHA WAANZISHA MAFUNZO BURE YA UDEREVA KWA VIJANA 110, WAFUNGUA MILANGO YA AJIRA

 POLISI ARUSHA WAANZISHA MAFUNZO BURE YA UDEREVA KWA VIJANA 110, WAFUNGUA MILANGO YA AJIRA

Na Joseph Ngilisho, ARUSHA

KATIKA hatua inayotajwa kuwa mkombozi kwa vijana wanaotoka katika mazingira magumu, Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limezindua rasmi mpango wa mafunzo maalum ya udereva bila malipo kwa washiriki 110, yakilenga kuwapa ujuzi wa kazi, leseni halali na kuwafungulia milango ya ajira na kujiajiri.

Mpango huo, ambao umeungwa mkono na vyuo mbalimbali vya udereva mkoani humo, unatajwa kuwa wa kwanza wa aina yake kwa kiwango hicho, ukiwalenga vijana ambao kwa muda mrefu walikosa uwezo wa kugharamia mafunzo ya udereva licha ya kuwa na ndoto za kujipatia kipato kupitia sekta ya usafirishaji.


Akizungumza Julai 27, 2026, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha, ACP Zauda Mohamed, alisema maandalizi yote muhimu yamekamilika na mafunzo yameanza rasmi baada ya kufikiwa kwa makubaliano na vyuo vya udereva vitakavyotekeleza programu hiyo.

Alisema Jeshi la Polisi limeweka mpango kazi madhubuti utakaohakikisha mafunzo hayo yanaendeshwa kwa ufanisi huku yakifuata sheria na taratibu zote zinazohitajika.

"Hatukuwataka vijana hawa wapate mafunzo pekee, bali tumewaandaa kuingia rasmi kwenye soko la ajira. Tayari wote wamepatiwa Namba ya Mlipa Kodi (TIN), Leseni ya Kujifunzia Udereva (Learner Licence) na wamesajiliwa kwenye mfumo wa usimamizi wa shule za udereva nchini," alisema ACP Zauda.

Kwa mujibu wake, washiriki hao watafundishwa kuendesha magari, pikipiki za magurudumu mawili na matatu pamoja na mitambo inayotumika viwandani na mashambani, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa zao za ajira katika sekta mbalimbali za uchumi.

ACP Zauda alisema mafanikio ya mpango huo yanategemea ushirikiano wa wadau mbalimbali, akitoa wito kwa taasisi, kampuni na watu binafsi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuwawezesha vijana na makundi mengine yenye uhitaji ili kujenga jamii inayojitegemea kiuchumi.

Mpango huo umepokelewa kwa shangwe na wamiliki wa vyuo vya udereva mkoani Arusha, waliompongeza Mkuu wa Usalama Barabarani kwa kubuni wazo hilo wakisema limegusa maisha ya vijana wengi waliokuwa wamekata tamaa ya kupata mafunzo ya udereva kutokana na gharama.

Walisema wako tayari kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika awamu zijazo ili kuhakikisha vijana wengi zaidi wanapata nafasi ya kujifunza na kujijengea maisha kupitia taaluma ya udereva.

Mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo alisema fursa hiyo imekuwa mwanzo mpya wa maisha yake, akieleza kuwa ujuzi atakaoupata utamwezesha kutafuta ajira au kujiajiri na kuboresha maisha yake pamoja na familia yake.

Mpango huo unahitimisha maandalizi yaliyofanywa kwa muda na sasa washiriki 110 wanaanza safari ya kujifunza taaluma ambayo inatarajiwa kubadili maisha yao na kuongeza nguvu kazi yenye ujuzi katika sekta ya usafirishaji nchini.








Ends

Post a Comment

أحدث أقدم