MAMA AKUMBWA NA MSIBA MZITO ARUSHA WATOTO WAKE WATANO WAFARIKI MMOJA BAADA YA MWINGINE MOUNT MERU AKIJIFUNGUA

MAMA AKUMBWA NA MSIBA MZITO ARUSHA WATOTO WAKE WATANO WAFARIKI MMOJA BAADA YA MWINGINE MOUNT MERU AKIJIFUNGUA

Na Joseph Ngilisho | Arusha

Simanzi na majonzi makubwa yameikumba familia moja jijini Arusha baada ya kupoteza watoto watano wa mapacha waliozaliwa kabla ya kutimiza muda wa kawaida wa ujauzito, huku wote wakifariki dunia mmoja baada ya mwingine walipokuwa wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru.

Tukio hilo la kusikitisha limetokea baada ya mama wa watoto hao, Bi. Careen Remmy, kupata uchungu usiku wa kuamkia Julai 26, 2026 na kukimbizwa hospitalini, ambako alijifungua salama kwa msaada wa madaktari.

Kwa mujibu wa mama huyo, furaha ya kuwapokea watoto wake ilidumu kwa muda mfupi tu baada ya madaktari kubaini kuwa walikuwa wamezaliwa njiti na kuhitaji uangalizi maalumu. Licha ya juhudi kubwa zilizofanywa na wataalamu wa afya, watoto hao walifariki dunia mmoja baada ya mwingine wakiwa katika kitengo cha uangalizi.

"Nashukuru Mungu kwa kunivusha salama wakati wa kujifungua. Madaktari walifanya kila walichoweza kuokoa maisha ya watoto wangu, lakini mapenzi ya Mungu yalikuwa tofauti," alisema mama huyo kwa sauti ya huzuni.

Baba wa watoto hao amesema alipokea habari za ujauzito wa mapacha watano kwa furaha isiyoelezeka na akaanza maandalizi ya kuwakaribisha duniani, akiamini wangekuwa sehemu ya baraka kubwa kwa familia yao.

"Tulikuwa na ndoto nyingi kuhusu watoto wetu. Tayari tulikuwa tunaanza maandalizi ya maisha yao, lakini leo tumebaki na majonzi makubwa. Hata hivyo, tunamshukuru Mungu na tunawashukuru madaktari na wauguzi kwa juhudi zote walizofanya," alisema.

Licha ya uchungu walioupata, wazazi hao wamesisitiza kuwa wahudumu wa afya wa Hospitali ya Mount Meru walionesha weledi na kujitolea katika kupigania maisha ya watoto hao hadi dakika za mwisho.

Naye babu wa watoto hao amesema familia imeanza maandalizi ya kuwaaga wajukuu hao, huku ikitarajia kuwazika katika kaburi moja eneo la Ilboru, jijini Arusha.

"Tumepokea pigo kubwa ambalo si rahisi kulielezea. Tunaendelea kumuomba Mungu atutie nguvu katika kipindi hiki kigumu, huku tukikamilisha maandalizi ya mazishi ya wajukuu wetu," alisema.

Tukio hilo limeguswa na wengi jijini Arusha, huku likiwa kumbusho la changamoto zinazoweza kujitokeza kwa watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao wa kawaida wa ujauzito na maumivu makubwa yanayoweza kuzikumba familia zinazopitia hali hiyo.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم