EXTRA LUXURY COACH YAZINDUA MABASI MANNE YA KISASA ARUSHA,YAISIMAMISHA ARUSHA, YAFUNGUA RUTI MPYA ZA GEITA NA MPANDA."

EXTRA LUXURY COACH YAZINDUA MABASI MANNE YA KISASA ARUSHA,YAISIMAMISHA ARUSHA, YAFUNGUA RUTI MPYA ZA GEITA NA MPANDA."

Na Joseph Ngilisho|ARUSHA

...Jiji la Arusha limelazimika kusimama kwa muda wakati kampuni ya Mabasi ya Extra Coach ikitambulisha vyuma vinne vipya kwa wakazi wa jiji hilo.

Katika Shangwe hilo,  chakula na vinywaji vilitawala katika ofisi za Extra Luxury Coach zilizopo eneo la Makao Mapya jijini Arusha, wakati kampuni hiyo ilipozindua rasmi mabasi manne mapya ya kisasa yaliyotarajiwa kuongeza ushindani katika sekta ya usafiri wa abiria nchini.

Hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi wa dini, wadau wa usafirishaji, wafanyabiashara na mamia ya wananchi, ilipambwa na maombi maalumu ya kuyaombea na kuyabariki mabasi hayo kabla ya kuanza kutoa huduma katika ruti mbalimbali za ndani ya Tanzania.

Kiongozi wa dini aliyeongoza ibada hiyo aliyaweka mabasi hayo chini ya ulinzi wa Mwenyezi Mungu, akiwaombea madereva, wahudumu na abiria wote watakaoyatumia wasafiri salama kila siku.


Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Extra Luxury Coach, Helmet Luka Masawe, alisema kampuni hiyo imeingia katika hatua mpya ya uwekezaji baada ya zaidi ya miaka 10 ya kutoa huduma za usafiri wa abiria, huku ikilenga kuwapa Watanzania usafiri wa kisasa, salama na wenye viwango vya juu.

Alisema mabasi hayo mapya yataanza kuhudumia ruti mpya ya Moshi–Arusha–Singida–Kahama–Katoro–Geita, sambamba na kuimarisha safari za kuelekea Mpanda kupitia Arusha, Singida na Tabora.

Mbali na ruti hizo, alisema kampuni itaendelea kutoa huduma katika safari za Moshi–Kahama–Ushirombo–Bukoba–Karagwe pamoja na Arusha–Moshi–Chalinze–Mbezi Makufuli na Mbagala, ikiwa sehemu ya mkakati wa kupanua mtandao wa usafiri nchini.

"Tumejipanga kuhakikisha kila abiria anayepanda basi la Extra Luxury Coach anapata huduma bora, salama na yenye hadhi. Uwekezaji huu ni mwanzo wa hatua nyingine kubwa ya kupanua huduma zetu nchini," alisema Masawe.

Katika hafla hiyo, wageni walijumuika kula na kunywa wakisherehekea mafanikio ya kampuni hiyo, huku wakieleza matumaini kuwa mabasi hayo mapya yataongeza ushindani, kuboresha huduma na kutoa chaguo zaidi kwa wasafiri wa mikoa ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa na Magharibi.

Uzinduzi wa mabasi hayo manne unaonyesha kasi ya uwekezaji unaoendelea katika sekta ya usafiri wa abiria, huku kampuni zikizidi kuwekeza katika mabasi ya kisasa yanayolenga kuongeza usalama, faraja na ufanisi wa safari kwa Watanzania.

Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم