EWURA YAWANOA MAAFISA TANESCO, MAMLAKA ZA MAJI KUIMARISHA HUDUMA KWA WATEJA


EWURA YAWANOA MAAFISA TANESCO, MAMLAKA ZA MAJI KUIMARISHA HUDUMA KWA WATEJA

Na Joseph Ngilisho | BABATI

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imechukua hatua mpya ya kuimarisha ubora wa huduma kwa wananchi kwa kuwajengea uwezo Maafisa wa Huduma kwa Wateja, Mahusiano na Sheria kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira za Kanda ya Kaskazini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma zenye weledi, uwazi na zinazozingatia matakwa ya sheria.

Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Hoteli ya White Rose mjini Babati, Mkoa wa Manyara, yalilenga kuongeza uelewa wa watendaji hao kuhusu namna bora ya kushughulikia malalamiko ya wananchi, kuwasiliana kwa ufanisi na wateja, pamoja na kuhakikisha huduma zote zinazotolewa zinaendana na sheria, kanuni na miongozo ya sekta za nishati na maji.

Akifungua semina hiyo, Meneja wa EWURA Kanda ya Kaskazini, George Mhina, alisema ubora wa huduma kwa wateja unategemea kwa kiasi kikubwa uwezo wa watendaji kuelewa wajibu wao na kutekeleza majukumu kwa uadilifu, weledi na kwa kuzingatia sheria.

Alisema maafisa wa huduma kwa wateja ndio sura ya kwanza ya taasisi wanazozitumikia, hivyo wanapaswa kuwa na uelewa wa kina wa masuala ya kisheria na kiudhibiti ili waweze kutoa majibu sahihi, ya haraka na yanayojenga imani kwa wananchi.

"Ni muhimu kila afisa afahamu wajibu wake na azingatie sheria na taratibu katika kushughulikia changamoto za wananchi. Hii ndiyo njia ya kujenga imani ya wateja na kuongeza ufanisi wa taasisi zetu," alisema Bw. Mhina.

Aliongeza kuwa EWURA itaendelea kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa wadau wake ili kuhakikisha viwango vya utoaji huduma vinaendelea kuimarika sambamba na matarajio ya wananchi na mabadiliko ya sera na sheria.

Kwa upande wao, washiriki wa semina hiyo walieleza kuwa mafunzo hayo yamewapa maarifa mapya yatakayowawezesha kuboresha utendaji wao na kushughulikia changamoto za wateja kwa ufanisi zaidi.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki, Devotha Mayala kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga alisema semina hiyo imewapa uelewa mpana kuhusu wajibu wa taasisi za huduma za umma katika kulinda haki za wateja na kuzingatia matakwa ya kisheria.

Naye Samwel Mandari kutoka TANESCO alisema mafunzo hayo yameimarisha uwezo wao wa kitaaluma na kuwapa mbinu bora za kushughulikia malalamiko ya wananchi kwa wakati, jambo litakaloongeza ufanisi wa utoaji huduma.

Semina hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa EWURA wa kuimarisha uwezo wa watoa huduma za nishati na maji nchini, huku ikiendelea kusimamia utekelezaji wa viwango vya huduma na kulinda maslahi ya watumiaji kupitia mfumo wa Udhibiti wa Haki kwa Matokeo Chanya, unaolenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na zenye kuzingatia haki zao.




Ends

Post a Comment

أحدث أقدم