TANGA YAVUKA MALENGO YA MAPATO KWA ASILIMIA 101, YATEKELEZA MIRADI 134 YA MAENDELEO

TANGA YAVUKA MALENGO YA MAPATO, YATEKELEZA MIRADI 134 YA MAENDELEO

Na Joseph Ngilisho | TANGA

HALMASHAURI ya Jiji la Tanga imeandika historia mpya ya utendaji kwa kuvuka malengo ya makusanyo kwa kukusanya bilioni 88.16 ikiwa ni sawa na asilimia 101 ya makisio ya bajeti ya mwaka 2025|26 na kuelekeza fedha hizo katika utekelezaji wa miradi 134 ya maendeleo iliyogusa sekta muhimu za afya, elimu, biashara, mazingira na miundombinu, hatua inayotajwa kubadilisha sura ya jiji hilo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Juma Hamsin, mafanikio hayo yametokana na kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani, usimamizi madhubuti wa rasilimali za umma na utekelezaji wa miradi yenye tija kwa wananchi.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, Halmashauri ilikusanya jumla ya Sh88.16 bilioni, sawa na asilimia 101 ya makisio ya Sh86.5 bilioni, huku mapato ya ndani yakifikia Sh19.91 bilioni, sawa na asilimia 103 ya lengo.

Kwa mujibu wa Hamsin, fedha hizo zimewezesha kutekelezwa kwa miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh9.38 bilioni, ambapo miradi 65 imekamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi, miradi 38 inaendelea, 16 ipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji, huku mingine ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Hamsin anaeleza kuwa uwekezaji huo umeongeza upatikanaji wa huduma za afya kupitia ujenzi wa vituo vya afya, majengo ya wagonjwa wa nje (OPD), nyumba za watumishi, huduma za X-Ray na kupunguza vifo vya wajawazito kutoka nane hadi vinne ndani ya mwaka mmoja.

Aidha, amesema sekta ya elimu imeimarishwa kupitia ujenzi wa madarasa ya ghorofa, shule mpya za sekondari, ununuzi wa zaidi ya viti na meza 13,000 na kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya taifa.

Hamsin amesema pamoja na mafanikio hayo, Halmashauri itaendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kukamilisha miradi inayoendelea na kuongeza uwekezaji katika huduma za kijamii ili kuifanya Tanga kuwa miongoni mwa majiji yanayoongoza nchini kwa utoaji wa huduma bora kwa wananchi. 

ends..

Post a Comment

أحدث أقدم