Ad
Breaking🔥

AJALI MBAYA YA BASI LA KANDAHARI MAKUYUNI YAUA 6, WENGI WAJERUHIWA

AJALI MBAYA YA BASI LA KANDAHARI MAKUYUNI YAUA WATU 6, WENGI WAJERUHIWA

Na Joseph Ngilisho|ARUSHA

 

 AJALI mbaya iliyohusisha basi la Kampuni ya Kandahari na malori mawili katika eneo la Makuyuni, Wilaya ya Monduli mkoani Arusha, imeua watu 6 na kujeruhi wengine kadhaa, huku hofu ikitanda kutokana na ukubwa wa maafa hayo.

Ajali hiyo ilitokea jana majira ya usiku wakati basi la Kandahari lenye namba za usajili T 732 DRL, lililokuwa likitoka Mkoa wa Kilimanjaro kuelekea Mpanda mkoani Katavi, lilipogongana uso kwa uso na semi-trela lenye namba T 727 EPW lililokuwa likitoka Kahama kuelekea Tanga kuchukua shehena ya saruji.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio, dereva wa basi alijaribu kulipita lori lililokuwa mbele yake katika eneo la kona, lakini kutokana na mwonekano hafifu wa barabara alijikuta akigongana ana kwa ana na semi-trela iliyokuwa ikitokea upande wa pili.

Nguvu ya mgongano huo ilisababisha uharibifu mkubwa wa basi, huku abiria wengi wakinaswa ndani ya chombo hicho. Dereva wa basi alifariki dunia papo hapo pamoja na abiria wengine wengi, huku majeruhi kadhaa wakikimbizwa hospitalini kwa matibabu.

Mashuhuda pia wamesema lori jingine lenye namba T 757 DWV, ambalo lilikuwa linafuatana na semi-trela hiyo, lilipinduka wakati dereva wake alipokuwa akijaribu kukwepa ajali hiyo.

Baada ya ajali, vikosi vya uokoaji vikishirikiana na Jeshi la Polisi, Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji pamoja na wasamaria wema vilifika eneo la tukio na kuanza kuwaokoa majeruhi, kutoa miili ya waliofariki na kuondoa magari yaliyoharibika yaliyokuwa yameziba barabara.

Ajali hiyo ilisababisha msongamano mkubwa wa magari katika Barabara Kuu ya Arusha–Babati kwa saa kadhaa wakati operesheni ya uokoaji ikiendelea.

Hadi taarifa hii inaandaliwa, Jeshi la Polisi lilikuwa bado halijatoa taarifa rasmi kuhusu idadi kamili ya waliofariki na majeruhi, likieleza kuwa uchunguzi unaendelea kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo na kuthibitisha takwimu rasmi za waathirika.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم