VIKUNDI 32 VYANUFAIKA NA MIKOPO YA ASILIMIA 10 NGORONGORO, MILIONI 180 ZATOLEWA
Na Joseph Ngilisho | Arushadigital, Ngorongoro
Jumla ya vikundi 32 vya wanawake na vijana katika Wilaya ya Ngorongoro vimenufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri, ambapo shilingi milioni 180 zimetolewa katika awamu ya nne mfululizo kwa lengo la kuimarisha shughuli za kiuchumi na kuongeza kipato kwa wanufaika.
Fedha hizo zimegawanywa kwa vikundi 17 vya vijana vilivyopatiwa shilingi milioni 96 na vikundi 15 vya wanawake vilivyopokea shilingi milioni 84. Vikundi hivyo vinajihusisha na shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ikiwemo ufugaji na unenepeshaji wa mifugo, kilimo pamoja na ufundi.
Akizungumza wakati wa hafla ya ugawaji wa mikopo hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, mwanachama wa Kikundi cha Faraja Digodigo, Bw. Noel Njuguna Kasone, amesema mikopo hiyo imekuwa nyenzo muhimu ya kukuza shughuli zao za uchomeleaji na utengenezaji wa samani za chuma.
Amesema utaratibu wa Serikali wa kutoa mikopo kwa wanawake na vijana umewasaidia wajasiriamali wadogo kuongeza mtaji na kupanua biashara zao.
"Ninamshukuru kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka utaratibu huu unaotuwezesha sisi wajasiriamali wadogo kupata mitaji ya kuendesha na kukuza shughuli zetu za kiuchumi. Mikopo hii imekuwa faraja kubwa na chachu ya maendeleo kwetu," amesema Kasone.
Naye Katibu wa Kikundi cha Naretu kutoka Kata ya Oloipiri, Narepo Munga, amesema mkopo huo usio na riba umechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya mradi wao wa unenepeshaji wa kondoo.
Amesema kutokana na nidhamu ya marejesho waliyoionesha, kikundi chao kimefanikiwa kunufaika na mkopo huo kwa mara ya tatu, jambo ambalo limewawezesha kuongeza uzalishaji na mapato.
"Tunashukuru Serikali kwa kuendelea kutuamini. Uwezo wetu wa kurejesha mikopo kwa wakati umetuwezesha kuendelea kupata fursa hii, ambayo imekuwa msaada mkubwa katika kukuza mradi wetu," amesema Munga.
Akiongoza hafla hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Mhe. Manja Yaile, alikabidhi hundi yenye thamani ya shilingi milioni 180 kwa vikundi 32 vilivyokidhi vigezo vya kupata mikopo hiyo.
Mhe. Yaile aliwataka wanufaika kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuhakikisha wanazingatia marejesho kwa wakati ili kutoa nafasi kwa vikundi vingine kunufaika na mfuko huo unaolenga kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi.
Mpango wa mikopo ya asilimia 10 umeendelea kuwa nyenzo muhimu ya Serikali katika kukuza uchumi wa wananchi kupitia uwezeshaji wa makundi maalumu, huku ukichochea ukuaji wa biashara ndogo ndogo na kuongeza ajira katika jamii.

Post a Comment