KAMATI YA BUNGE YAPENDEKEZA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA KUWA HOSPITALI YA TAIFA

 KAMATI YA BUNGE YAPENDEKEZA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA KUWA HOSPITALI YA TAIFA

Na Arushadigital -DODOMA 

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imeipendekeza Serikali kuipandisha hadhi Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kutoka hospitali ya rufaa ya kanda na kuwa Hospitali ya Taifa, kutokana na uwezo mkubwa iliofikia katika utoaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi nchini. 

Mapendekezo hayo yalitolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Johannes Lukumay, wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.

Dkt. Lukumay alisema wajumbe wa kamati hiyo wameridhishwa na maendeleo makubwa yaliyofikiwa na hospitali hiyo, hususan katika utoaji wa huduma 20 za kibingwa na huduma 17 za ubingwa bobezi, zikiwemo huduma za upandikizaji wa figo na upandikizaji wa uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa selimundu.


Alisema kiwango cha huduma zinazotolewa kwa sasa kinaifanya hospitali hiyo kustahili kuwa Hospitali ya Taifa, hatua ambayo itapanua upatikanaji wa matibabu ya kisasa kwa Watanzania wengi na kupunguza gharama kubwa zinazotumika kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu.

“Hospitali hii imeonyesha uwezo mkubwa wa kutoa huduma za kibingwa na bobezi ambazo hapo awali zilikuwa zinapatikana nje ya nchi. Tunaamini hadhi ya Hospitali ya Taifa itaongeza uwezo wake wa kuwahudumia Watanzania wengi zaidi,” alisema Dkt. Lukumay. 

Mbali na pendekezo hilo, kamati hiyo pia imeishauri Serikali kuendelea kuimarisha mfumo wa bima ya afya kwa wote pamoja na kuwekeza katika viwanda vya ndani vya kuzalisha dawa na vifaa tiba ili kupunguza gharama za matibabu na utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi. 

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, alisema Serikali itaendelea kuhakikisha ujenzi wa Kituo cha Umahiri na Mafunzo ya Saratani katika Hospitali ya Benjamin Mkapa unakamilika kwa wakati pamoja na kusimikwa kwa vifaa muhimu ili kuwezesha utoaji wa huduma za kibingwa za saratani katika maeneo mbalimbali nchini.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi, alisema hospitali hiyo imepiga hatua kubwa kutokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika miundombinu, vifaa tiba na rasilimali watu.

Prof. Makubi alisema zaidi ya asilimia 60 ya huduma za kibingwa na ubingwa bobezi zilizopangwa tayari zimeanza kutolewa hospitalini hapo, hali iliyosaidia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi na kuifanya hospitali hiyo kuwa kituo muhimu cha matibabu ya kibingwa nchini. 

Hospitali ya Benjamin Mkapa imeendelea kujijengea sifa kama moja ya vituo vinavyoongoza nchini katika utoaji wa huduma za afya za kiwango cha juu, ikiwemo upandikizaji wa figo, upandikizaji wa uloto, matibabu ya moyo na huduma nyingine za ubingwa bobezi ambazo zimekuwa zikiwasaidia maelfu ya Watanzania kupata matibabu ndani ya nchi. 

Hatua ya kuipandisha hadhi hospitali hiyo kuwa Hospitali ya Taifa inatajwa kuwa inaweza kuimarisha zaidi sekta ya afya nchini kwa kuongeza uwezo wa huduma za rufaa na kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi. 

Post a Comment

Previous Post Next Post