MAKALA ATAKA BARABARA YA LOSINYAI–TANGANYIKA PACKERS–MBAUDA IKAMILIKE KABLA YA AFCON 2027

MAKALLA ATAKA BARABARA YA LOSINYAI–TANGANYIKA PACKERS–MBAUDA IKAMILIKE KABLA YA AFCON 2027

Na Joseph Ngilisho, Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, ameagiza kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Barabara ya Losinyai–Tanganyika Packers–Mbauda pamoja na mradi wa usimikaji wa taa katika Uwanja wa Ndege wa Arusha ili ikamilike kwa wakati, kuelekea maandalizi ya Mkutano wa Jumuiya ya Mabunge Duniani (IPU) na Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027.

Makalla alitoa maagizo hayo Juni 22, 2026, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya miradi hiyo mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa mkoani Arusha kwa lengo la kuboresha miundombinu ya usafiri na kuchochea ukuaji wa uchumi.


Akizungumza baada ya kukagua mradi wa usimikaji taa katika Uwanja wa Ndege wa Arusha, Makalla alisema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa ya utekelezaji wa mradi huo ambao umegharimu zaidi ya Shilingi bilioni 11 zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Alisema kukamilika kwa mradi huo kutaufanya uwanja huo kuanza kutoa huduma kwa saa 24 kuanzia mwezi Agosti mwaka huu, hatua itakayoongeza ufanisi wa usafiri wa anga, kukuza sekta ya utalii na kuimarisha shughuli za biashara katika Kanda ya Kaskazini.

“Rais Samia ametenga fedha nyingi kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa wakati. Dhamira yake ni kuona Uwanja wa Ndege wa Arusha unafanya kazi usiku na mchana ili kuongeza fursa za kiuchumi na kuimarisha huduma za usafiri wa anga. Tunatarajia mradi ukabidhiwe rasmi ifikapo Agosti Mosi mwaka huu,” alisema Makalla.

Aliongeza kuwa vifaa vilivyosalia kwa ajili ya kukamilisha mradi huo vinatarajiwa kuwasili mkoani humo kuanzia Juni 23, 2026, jambo litakaloharakisha hatua za mwisho za utekelezaji.

Katika ukaguzi wa mradi wa Barabara ya Losinyai–Tanganyika Packers–Mbauda, Makalla alieleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi, lakini akazitaka taasisi na mashirika ya umma zenye miundombinu ndani ya eneo la mradi kushirikiana na mkandarasi ili kuondoa vikwazo vinavyoweza kuchelewesha kazi.

Aliielekeza TANESCO pamoja na mamlaka za maji kuondoa kwa haraka nguzo za umeme na miundombinu mingine iliyopo ndani ya eneo la ujenzi ili kutoa nafasi kwa mkandarasi kuendelea na kazi kwa ufanisi.

“TANESCO na mamlaka za maji wahakikishe wanaondoa miundombinu yao kwa wakati. Serikali tayari imeshatoa malipo ya awali na hakuna sababu ya kuchelewesha utekelezaji wa mradi huu muhimu. Pia nitumie nafasi hii kumshukuru Rais Samia kwa uwekezaji mkubwa wa miundombinu unaoendelea Arusha,” alisema.

Alibainisha kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutakuwa suluhisho muhimu la kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Arusha, sambamba na kuimarisha mtandao wa usafiri kuelekea AFCON 2027.

Kwa upande wake, Mkandarasi Mkazi wa Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), Liu Nanjing, aliahidi kukamilisha mradi huo kwa wakati uliopangwa, akisema kampuni hiyo imejipanga kuongeza kasi ya ujenzi huku ikiendelea kutoa ajira kwa vijana wa Mkoa wa Arusha.

Alisema barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 70 ni miongoni mwa miradi muhimu ya miundombinu inayotekelezwa kwa viwango vya kisasa na itakuwa na mchango mkubwa katika kuboresha huduma za usafiri na maendeleo ya kiuchumi ya mkoa huo.

Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post