NDANGIZA AMSIFIA KATIBU MKUU MPYA, ATAKA UMOJA WA TAASISI ZA EAC

NDANGIZA AMSIFIA KATIBU MKUU MPYA, ATAKA UMOJA WA TAASISI ZA EAC

Na Joseph Ngilisho- ARUSHA 

MBUNGE wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), Fatuma Ndangiza, ametoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na vyombo vingine vya Jumuiya hiyo, akisisitiza kuwa mshikamano wa taasisi ndicho chachu ya mafanikio ya ajenda ya ukanda.

Akichangia mjadala katika kikao cha Bunge la EALA, Ndangiza alisema ana matumaini makubwa na uongozi wa Katibu Mkuu wa EAC, akibainisha kuwa kauli zake za kujitambulisha kama “Katibu Mkuu wa Jumuiya yote” zinaonyesha dhamira ya kuunganisha taasisi na wananchi wa Afrika Mashariki.

Alisema mafanikio ya nguzo nne za ushirikiano wa kikanda—ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi, kijamii na kimkakati—yanaweza kupatikana tu endapo kila taasisi itatekeleza wajibu wake kikamilifu kwa kushirikiana bila mipaka ya kiutendaji.

“Endapo Sekretarieti itafanya kazi kikamilifu huku taasisi nyingine zikiwa hazishiriki ipasavyo katika majukumu yao ya uwakilishi, kutunga sheria na usimamizi, basi malengo ya Jumuiya hayatakamilika,” alisema Ndangiza.

Ameongeza kuwa ucheleweshaji wa haki kutokana na changamoto katika Mahakama ya Jumuiya unaleta madhara kwa wananchi, akisisitiza kuwa haki iliyochelewa ni sawa na haki kunyimwa.

Katika mchango wake, alitoa pendekezo la Katibu Mkuu wa EAC kukutana rasmi na EALA angalau mara mbili kwa mwaka ili kujadili masuala ya kiutendaji na kuimarisha uhusiano wa kikazi.

Aidha, ameitaka Sekretarieti kushirikiana na Bunge katika kupanga mikutano ya pamoja ya kimkakati (retreats) kati ya Baraza la Mawaziri, Sekretarieti na Bunge hilo ili kutatua changamoto zinazoikabili Jumuiya kwa njia ya majadiliano.

Ndangiza pia alisisitiza umuhimu wa usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake, akisema kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wananchi wa Afrika Mashariki ni wanawake, hivyo maendeleo endelevu hayawezi kupatikana bila kuwashirikisha kikamilifu.

Alimalizia kwa kuipongeza Sekretarieti kwa dhamira yake ya kuunga mkono majukumu ya usimamizi ya Bunge, hususan katika kuhakikisha miradi yote ya East African Community inafanyiwa uangalizi wa karibu na wa kina.

“Tunataka ushirikiano wa karibu zaidi kati ya taasisi zote za Jumuiya ili kuwaletea wananchi wa Afrika Mashariki matokeo ya kweli ya maendeleo,” alihitimisha.


...ENDS..

Post a Comment

Previous Post Next Post