MILLYA AZITAKA NCHI WANACHAMA KUTEKELEZA WAJIBU WAO WA KIFEDHA EAC

 MILLYA AZITAKA NCHI WANACHAMA KUTEKELEZA WAJIBU WAO WA KIFEDHA EAC

Na Joseph Ngilisho, ARUSHA 

NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Ole Millya, ametoa wito kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuhakikisha zinatimiza wajibu wao wa kuchangia fedha za Jumuiya kwa wakati ili kuwezesha utekelezaji wa shughuli na miradi ya maendeleo ya kikanda.


Akizungumza katika kikao cha Bunge la jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) kinachoendelea katika Makao Makuu ya EAC jijini Arusha Leo Juni 22,2026, Millya alisema ucheleweshaji wa michango kutoka kwa baadhi ya nchi wanachama umekuwa changamoto inayokwamisha utekelezaji wa mipango na programu mbalimbali za Jumuiya.


Alisema Baraza la Mawaziri la EAC linaendelea kusisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuheshimu wajibu wao kwa mujibu wa Mkataba wa EAC, huku likitumia njia mbalimbali za kidiplomasia kuhakikisha michango hiyo inawasilishwa kwa wakati.


Millya pia aliwataka wabunge wa EALA kutumia nafasi na ushawishi wao katika nchi zao kuhamasisha serikali kutekeleza wajibu huo kwa hiari na kwa wakati, akieleza kuwa mafanikio ya Jumuiya yanategemea ushirikiano na uwajibikaji wa kila nchi mwanachama.


“Ninawaomba waheshimiwa wabunge kutumia mahusiano yenu mazuri na viongozi wa nchi zenu kuhimiza utekelezaji wa wajibu huu muhimu. EAC inahitaji rasilimali za kutosha ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi,” alisema.


Aidha, alimhakikishia Katibu Mkuu wa EAC kuwa Baraza la Mawaziri litaendelea kutoa ushirikiano wa karibu katika kutafuta suluhisho la changamoto za kifedha zinazoikabili Jumuiya na kuhakikisha taasisi zake zinafanya kazi kwa ufanisi.


Millya alisema Baraza la Mawaziri lina dhamira ya dhati ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kusukuma mbele ajenda za maendeleo zinazolenga kuwanufaisha wananchi wa Afrika Mashariki.


Aliongeza kuwa mapendekezo na maoni yaliyotolewa na wabunge wa EALA yamepokelewa na yatafanyiwa kazi, huku Baraza likiahidi kutoa mrejesho kuhusu hatua zitakazochukuliwa katika kutekeleza hoja mbalimbali zilizowasilishwa bungeni.


Alisisitiza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya Baraza la Mawaziri, Sekretarieti ya EAC na Bunge la EALA ni msingi muhimu katika kuimarisha mshikamano na maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.


Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post