MAHERA AUNGA MKONO BAJETI YA SERIKALI KWA ASILIMIA 100, AIPONGEZA KWA KUJENGA UCHUMI JUMUISHI
Na Joseph Ngilisho-Arushadigital|DODOMA
Mbunge wa Butiama, Dkt. Charles Mahera, ameunga mkono kwa asilimia 100 Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027, akisema imebeba mwelekeo sahihi wa kukuza uchumi jumuishi, kuimarisha viwanda vya ndani na kuongeza ustawi wa wananchi kupitia matumizi makubwa ya mapato ya ndani.
Akichangia mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali bungeni jijini Dodoma, Dkt. Mahera alianza kwa kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Butiama kwa kumwamini na kumpa nafasi ya kuwawakilisha bungeni, huku akiipongeza Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji kwa kuwasilisha bajeti aliyosema inalenga kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii.
“Naanza kwa kuwashukuru wananchi wa Butiama kwa kunipa fursa ya kuwawakilisha hapa bungeni. Aidha, naipongeza Serikali yetu kwa kuandaa bajeti nzuri ambayo inalenga kukuza uchumi wa taifa na kuboresha maisha ya wananchi. Nimeamua kuiunga mkono kwa asilimia mia moja,” alisema.
Alisema bajeti hiyo imejengwa katika misingi ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 na inalenga kuifanya Tanzania kuwa taifa lenye uchumi imara na linalojitegemea.
Dkt. Mahera alibainisha kuwa ongezeko la mapato ya Serikali hadi kufikia Sh trilioni 62.33 ni ishara ya kuimarika kwa uwezo wa nchi kujitegemea kifedha, huku mapato ya ndani yakifikia Sh trilioni 46.79.
“Zaidi ya asilimia 74 ya bajeti hii inategemea mapato ya ndani. Hii inaonyesha wazi kuwa Serikali inaendelea kupunguza utegemezi wa misaada ya nje na kujenga uchumi unaotegemea nguvu zake yenyewe,” alisema.
Mbunge huyo alisema bajeti hiyo imezingatia mahitaji ya makundi mbalimbali ya wananchi, ikiwemo vijana, wafanyabiashara wadogo na wamachinga, ambao wamewekewa mazingira bora ya kiuchumi kupitia kuongezwa kwa fedha katika Mfuko wa Wamachinga.
Alisema hatua ya kuongeza fedha katika mfuko huo itawawezesha wafanyabiashara wadogo kupata mikopo na kuimarisha biashara zao, jambo litakalosaidia kupanua wigo wa ajira na kuongeza mapato ya wananchi.
Kwa upande wa afya, Dkt. Mahera aliipongeza Serikali kwa kutenga vyanzo vya fedha vitakavyowezesha utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, akisema hatua hiyo itawapa wananchi wa kipato cha chini fursa ya kupata huduma bora za afya bila vikwazo vya kifedha.
“Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya kwa wakati. Hili ni jambo la kupongezwa kwa kuwa linaimarisha ustawi wa wananchi,” alisema.
Aidha, aliunga mkono marekebisho ya sheria mbalimbali yaliyowasilishwa sambamba na bajeti hiyo, akisema yatasaidia kurasimisha sekta isiyo rasmi na kuwapa wafanyabiashara wadogo nafasi ya kuingia kwenye mfumo rasmi wa kodi bila kuathiri shughuli zao za kiuchumi.
Katika sekta ya kilimo na viwanda, Dkt. Mahera alisema kuondolewa kwa baadhi ya tozo kwenye mafuta ya alizeti yanayozalishwa nchini pamoja na bidhaa zinazotokana na pamba kutachochea uzalishaji wa mazao hayo na kuongeza thamani ya mazao ya wakulima.
Alisema hatua hiyo ni muhimu kwa mikoa inayozalisha pamba na alizeti, kwani itapanua soko la mazao hayo na kuongeza uzalishaji wa viwanda vinavyotumia malighafi za ndani.
Mbali na hayo, mbunge huyo aliipongeza Serikali kwa hatua zake za kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa kuondoa tozo kwenye vifaa vya kuchaji magari ya umeme pamoja na mita janja za matumizi ya gesi ya kupikia.
Alisema hatua hizo zitachangia kupunguza utegemezi wa nishati zinazochafua mazingira na kuharakisha utekelezaji wa mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Bajeti hii imegusa wananchi wa kada zote. Inajenga uchumi, inaimarisha huduma za kijamii, inaongeza fursa za ajira na wakati huo huo inalinda mazingira. Kwa sababu hizo, naiunga mkono kwa asilimia mia moja,” alisema Dkt. Mahera.
**Ends**

إرسال تعليق