BEI ZA MAFUTA ZAANZA KUTEREMKA DUNIANI KADRI MATUMAINI YA AMANI MASHARIKI YA KATI YAKIONGEZEKA
Na Arushadigital
Mataifa mbalimbali duniani yameanza kupata afueni baada ya bei za mafuta katika soko la dunia kuanza kushuka kufuatia kuongezeka kwa matumaini ya kumalizika kwa mzozo wa Mashariki ya Kati uliotikisa uchumi wa dunia kwa miezi kadhaa.
Hatua hiyo imekuja baada ya Marekani na Iran kutangaza mwanzoni mwa wiki kuwa zimefikia makubaliano ya kusitisha mapigano na kurejesha shughuli za kawaida za usafirishaji wa nishati kupitia Mlango Bahari wa Hormuz, njia muhimu inayopitisha takribani asilimia 20 ya mafuta na gesi inayotumika duniani.
Kutokana na maendeleo hayo, bei ya mafuta ghafi imeanza kushuka kwa kasi katika soko la kimataifa. Leo Jumanne, pipa moja la mafuta ghafi limeuzwa kwa wastani wa dola za Marekani 78, ikilinganishwa na karibu dola 120 kwa pipa zilizorekodiwa miezi miwili iliyopita wakati wa kilele cha mvutano huo.
Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanaeleza kuwa kushuka kwa bei hizo kunaweza kusaidia kupunguza gharama za usafiri, uzalishaji na maisha kwa ujumla katika mataifa mengi yaliyokuwa yameathiriwa na ongezeko la gharama za nishati.
Maendeleo hayo yanajiri siku moja tu baada ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuonya kuwa kuendelea kupanda kwa bei za mafuta kungeweza kuhatarisha ustawi wa uchumi wa mataifa yanayoendelea na kuongeza presha ya mfumuko wa bei.
Nchi kadhaa za Afrika, zikiwemo Tanzania na Rwanda, zimekuwa miongoni mwa zilizoathiriwa zaidi na kupanda kwa bei za mafuta tangu kuzuka kwa vita hivyo mwezi Februari 2026, ambapo bei za bidhaa za mafuta ziliongezeka kwa takribani asilimia 50 na kusababisha kupanda kwa gharama za usafirishaji na maisha ya wananchi.
Hata hivyo, kushuka kwa bei za mafuta kunatoa matumaini mapya kwa serikali na wananchi kwamba gharama za nishati zinaweza kuanza kurejea katika viwango vya kawaida iwapo amani itaendelea kudumu katika eneo hilo muhimu kwa uchumi wa dunia.

إرسال تعليق