BODABODA WAPANDISHA JENEZA JUU YA GARI LA DC KUSHINIKIZA WENZAO WAACHIWE
Na Arushadigital|Siha
Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dkt. Christopher Timbuka, ametoa ufafanuzi kuhusu tukio la kundi la waendesha pikipiki (bodaboda) kupandisha jeneza lenye mwili wa marehemu Emmanuel Mwanri juu ya gari la Mkuu wa Wilaya wakati wa shughuli za mazishi wilayani humo.
Dkt. Timbuka amesema tukio hilo lilitokana na juhudi za baadhi ya waendesha bodaboda kushinikiza kuachiwa kwa wenzao 10 waliokuwa wamekamatwa na Jeshi la Polisi kwa kukaidi maelekezo ya kutofanya msafara wa pikipiki wakati wa kusafirisha mwili wa marehemu.
Alieleza kuwa marehemu Emmanuel Mwanri alifariki dunia Juni 12, 2026 katika Wilaya ya Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro, na wakati wa maandalizi ya mazishi, vyombo vya usalama vilitoa maelekezo ya kuzuia misafara hiyo ili kuepusha usumbufu kwa watumiaji wengine wa Barabara ya Moshi–Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Juni 17, 2026, Dkt. Timbuka alisema baadhi ya waendesha bodaboda walichukua hatua ya kupandisha jeneza hilo juu ya gari la Mkuu wa Wilaya kama njia ya kuishinikiza Serikali na vyombo vya usalama kuwaachia wenzao waliokuwa wanashikiliwa.
Hata hivyo, alisema Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na familia ya marehemu ilifanikiwa kudhibiti hali hiyo na kurejesha utulivu, hali iliyowezesha shughuli za mazishi kuendelea na mwili wa marehemu kuzikwa salama katika nyumba yake ya milele.
Dkt. Timbuka amewataka wananchi kuendelea kuheshimu sheria, taratibu na maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika, akisisitiza kuwa hatua zote zinazochukuliwa na vyombo vya usalama zinalenga kulinda usalama wa wananchi na watumiaji wa barabara.
Ends..


إرسال تعليق