GAMBO ATAMBA MIRADI MIKUBWA ARUSHA NI MATUNDA YA UONGOZI WAKE, ATAKA MBUNGE WA SASA APIMWE BAADA YA MIAKA MITANO

GAMBO ATAMBA MIRADI MIKUBWA ARUSHA NI MATUNDA YA UONGOZI WAKE, ATAKA MBUNGE WA SASA APIMWE BAADA YA MIAKA MITANO

Na Joseph Ngilisho | Arusha

ALIYEKUWA Mbunge wa Arusha Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Mrisho Gambo, amesema miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa katika Jiji la Arusha ikiwemo ujenzi wa uwanja wa mpira wa AFCON, ni matokeo ya maono, mipango na juhudi za uongozi wake pamoja na Bunge lililopita, akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kupimwa kwa matokeo ya miaka mitano ya utumishi wao na si kwa ujanja ujanja.

Gambo amesema ni mapema kumhukumu au kumlinganisha mbunge wa sasa wa Arusha Mjini na viongozi waliopita, akieleza kuwa tathmini sahihi ya uwezo wa kiongozi hufanyika baada ya kukamilika kwa kipindi chake cha uongozi. Alidai kuwa miradi mingi inayoshuhudiwa leo jijini humo ilianza kuandaliwa, kupigiwa debe na kufuatiliwa wakati akiwa mbunge wa jimbo hilo.

Kauli hiyo aliitoa Jumapili, Juni 21, 2026, alipokuwa mgeni rasmi katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Makao Makuu ya Kanisa la Pentecoste Revival Church jijini Arusha, ambapo pamoja na masuala ya maendeleo, alizungumzia pia umuhimu wa haki, maridhiano na amani katika ujenzi wa Taifa.

Akizungumza mbele ya mamia ya waumini na wananchi waliohudhuria harambee hiyo, Gambo alisema tangu alipoachwa katika mchakato wa kuwania ubunge hakuwahi kujitokeza hadharani kutoa kauli yoyote kuhusu siasa za jimbo hilo, akieleza kuwa alichagua kunyamaza kwa kuwa wakati mwingine kimya ni jibu lenye nguvu kuliko maneno.

Alisema kama muumini wa dini ya Kiislamu anaamini kila jambo linalotokea katika maisha ya mwanadamu lina sababu na kwamba wajibu wa kwanza ni kumshukuru Mungu katika kila hali. Hata hivyo, alibainisha kuwa ukimya wake haukumaanisha ameacha kufuatilia maendeleo ya Arusha na Taifa kwa ujumla.

Katika hotuba yake, Gambo alisisitiza kuwa amani inayohubiriwa nchini haiwezi kudumu bila kuwepo kwa haki, akieleza kuwa msingi mkuu wa maridhiano ya kweli ni kuhakikisha wananchi wanatendewa haki katika nyanja zote za maisha yao. Aliongeza kuwa pale haki inapokosekana, manung'uniko, migawanyiko na kutokuaminiana hujitokeza katika jamii.

“Mtu yoyote anayehubiri amani lazima aanze na haki. Mahali ambapo kuna haki, hapatakuwa na manung'uniko. Amani ni tunda la haki,” alisema Gambo huku akipigiwa makofi na washiriki wa harambee hiyo.

Mwanasiasa huyo aliongeza kuwa maridhiano yanayoendelea kuzungumzwa nchini yanapaswa kujengwa juu ya ukweli, nia njema na dhamira ya dhati ya kulirejesha Taifa katika misingi ya upendo, mshikamano na umoja wa kitaifa. Alisema wananchi wanahitaji kuona vitendo vinavyodhihirisha haki badala ya kauli pekee.

Aidha, aliwashukuru wananchi wa Arusha Mjini kwa imani waliyoonyesha kwake kwa kumchagua kuwa mbunge kwa kipindi cha miaka mitano, akisema muda huo ulimwezesha kushiriki kusukuma ajenda mbalimbali za maendeleo ambazo leo zinaendelea kuwanufaisha wakazi wa jiji hilo.

Gambo alitumia fursa hiyo kueleza kuwa uongozi si suala la ujanja, mbinu za kisiasa au nguvu za kifedha, bali ni wito wa Mungu wa kuwatumikia watu. Alisema viongozi wanaofanikiwa kuacha alama ni wale wanaoweka mbele maslahi ya wananchi na maendeleo ya Taifa kuliko maslahi yao binafsi.

Katika harambee hiyo, jumla ya Shilingi 116,206,000 zilipatikana kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa Makao Makuu ya Kanisa hilo. Gambo alichangia Shilingi milioni 10, huku taasisi mbalimbali zikiwemo wadau wa maendeleo wakijitokeza kuchangia kufanikisha mradi huo wa kidini.

Akihitimisha hotuba yake, aliwataka viongozi wa dini kuendelea kuwa nguzo muhimu ya kulinda amani, maadili na mshikamano wa Taifa kwa kuhubiri haki, upendo na uwajibikaji, akisisitiza kuwa ujenzi wa Taifa bora ni jukumu la kila Mtanzania bila kujali tofauti za kisiasa, kidini au kijamii.

Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم