KATIBU MKUU EAC,AOMBA USHIRIKIANO ANZA MAZUNGUMZO NA WAKUU WA NCHI KUSAKA MICHANGO YA NCHI WANACHAMA INAYOSUASUA, NDANGIZA AMPONGEZA
Na Joseph Ngilisho– ARUSHA
KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Balozi Steven Mbundi, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za Jumuiya hiyo na nchi wanachama ili kuhakikisha EAC inatekeleza kikamilifu majukumu yake ya msingi ya kuleta maendeleo na ustawi wa wananchi wa ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza leo Juni 22,2026 katika kikao cha Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki EALA kinachoendelea katika makao makuu ya EAC jijini Arusha, Mbundi alisema mafanikio ya Jumuiya hiyo yanategemea mshikamano wa kweli kati ya Sekretarieti, Baraza la Mawaziri, Bunge la EALA na Serikali za nchi wanachama.
Alisema yeye na timu yake wamejipanga kikamilifu kutekeleza majukumu yao, lakini akasisitiza kuwa Sekretarieti haiwezi kufanikiwa pekee bila ushirikiano wa taasisi zote, akieleza kwa msisitizo kuwa “sisi ni timu moja na tunapaswa kufanya kazi kwa pamoja.”
Katika hatua nyingine, Mbundi alibainisha kuwa tayari ameanza mazungumzo na baadhi ya Wakuu wa Nchi wanachama, wakiwemo Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Rais Paul Kagame, kuhusu changamoto ya michango ya nchi wanachama ambayo imekuwa kikwazo cha muda mrefu katika utekelezaji wa mipango ya Jumuiya hiyo.
Alisema viongozi hao wameonyesha dhamira ya dhati ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuendeleza ajenda ya muungano wa Afrika Mashariki, huku akibainisha kuwa maono yao ya uunganishaji wa kikanda yako mbele zaidi kuliko kiwango cha utekelezaji kilichopo katika baadhi ya taasisi.
Kwa mujibu wa Mbundi, suala la michango ya nchi wanachama limepokelewa kwa mtazamo chanya na linaendelea kupewa kipaumbele katika majadiliano ya kikanda ili kuhakikisha shughuli za Jumuiya hazikwami.
Akiwashukuru wajumbe wa EALA kwa pongezi na ushirikiano, Mbundi alisema jukumu alilopewa ni zito lakini yuko tayari kulibeba, akisisitiza: “Mzigo huu ni mzito, lakini niko tayari kuubeba.”
Kwa upande wake, Mbunge wa EALA, Fatuma Ndangiza, ameitaka Sekretarieti na taasisi nyingine za Jumuiya hiyo kuimarisha ushirikiano wa kiutendaji ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa ajenda ya kikanda.
Akichangia mjadala katika kikao hicho, Ndangiza alisema ana matumaini makubwa na uongozi wa Katibu Mkuu Mbundi, akibainisha kuwa msisitizo wake wa kuiona Sekretarieti kama “Katibu Mkuu wa Jumuiya yote” ni ishara ya dhamira ya kuunganisha taasisi na wananchi.
Alisema mafanikio ya nguzo nne za ushirikiano wa kikanda—kisiasa, kiuchumi, kijamii na kimkakati—yanawezekana tu endapo kila taasisi itatekeleza majukumu yake kikamilifu kwa kushirikiana bila mipaka ya kiutendaji.
Ndangiza pia alisisitiza kuwa ucheleweshaji wa haki kupitia changamoto za Mahakama ya Jumuiya unaleta athari kwa wananchi, akisema “haki iliyochelewa ni sawa na haki kunyimwa.”
Alipendekeza Katibu Mkuu wa EAC kukutana rasmi na Bunge la EALA angalau mara mbili kwa mwaka kwa ajili ya kujadili masuala ya kiutendaji, pamoja na kuanzisha vikao vya pamoja vya kimkakati kati ya Sekretarieti, Baraza la Mawaziri na Bunge ili kutatua changamoto za Jumuiya kwa majadiliano ya pamoja.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa usawa wa kijinsia, akibainisha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wananchi wa Afrika Mashariki ni wanawake, hivyo maendeleo endelevu hayawezi kupatikana bila ushiriki wao kamili.
“Tunataka ushirikiano wa karibu zaidi kati ya taasisi zote za Jumuiya ili kuwaletea wananchi matokeo ya kweli ya maendeleo,” alihitimisha Ndangiza.
...Ends....

إرسال تعليق