MWENYEKITI WA HALMASHAURI AISISITIZA UTEKELEZAJI WA MAADHIMIO YA BARAZA LA MADIWANI ARUSHA DC

 BARAKA SIMION AISISITIZA UTEKELEZAJI WA MAADHIMIO YA BARAZA LA MADIWANI ARUSHA DC

Na Joseph Ngilisho-|ARUMERU

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha(Arusha DC), Baraka Mesiaki amesisitiza umuhimu wa Halmashauri hiyo kuhakikisha inafanyia kazi maadhimio yote yanayotolewa na Baraza la Madiwani kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya wananchi katika sekta mbalimbali.


Akizungumza leo katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Arusha DC, Baraka alisema ni muhimu kwa Mkurugenzi WA Halmashauri pamoja na idara zote kuendelea kusimamia utekelezaji wa maazimio, mapendekezo na ushauri unaotolewa na madiwani kwa manufaa ya wananchi.

“Ninaamini hata haya tunayoyaona leo ni mwendelezo wa kazi ile ile tuliyoianza. Maana yake Kurugenzi na idara zote mmeendelea kuhakikisha yale tuliyoshauri, tuliyopendekeza na kuyaelekeza yanafanyiwa kazi kwa vitendo,” alisema.

Aidha, aliipongeza Halmashauri hiyo kwa utekelezaji mzuri wa maadhimio yaliyotolewa katika vikao vya nyuma vya Baraza la Madiwani, akisema hatua hiyo imeendelea kuleta matokeo chanya katika sekta za elimu, afya, maji, barabara pamoja na miundombinu mingine ya maendeleo.

Baraka alisema usikivu wa wataalamu wa halmashauri pamoja na ushirikiano uliopo kati ya madiwani na watendaji umechangia kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayowanufaisha wananchi wa Arusha DC.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri pamoja na timu yake kwa kuendelea kusimamia miradi ya kimkakati yenye lengo la kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri hiyo, ikiwemo ujenzi wa soko la Kisongo, apartments pamoja na hoteli.

“Tuliona halmashauri nyingine zina vitega uchumi vikubwa vinavyozisaidia kujiendesha. Leo na sisi tunaona hatua kubwa zikianza kuchukuliwa na tunaamini Arusha DC itaendelea kuwa miongoni mwa halmashauri zenye uwezo mkubwa wa kujitegemea,” alisema.

Aidha, aliwataka wataalamu wa halmashauri hiyo kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo pamoja na sekta binafsi ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa wakati na kuleta tija kwa wananchi.

Katika kikao hicho, Baraka pia aliibua changamoto ya muda mrefu ya maji yenye kiwango kikubwa cha fluoride katika maeneo ya Rujewa na Oldonyo Sambu, akitaka wananchi wa maeneo hayo kupatiwa majibu ya uhakika kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji inayolenga kuondoa changamoto hiyo.

“Wananchi wetu wanaendelea kupata madhara makubwa kutokana na maji yenye fluoride. Serikali lazima iendelee kutoa majibu ya uhakika ili wananchi waendelee kuwa na imani nayo,” alisema.

Kwa upande wa miundombinu ya barabara, aliipongeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wilaya, TARURA pamoja na Halmashauri kwa kuanza matengenezo ya baadhi ya barabara zilizoharibiwa na mvua za masika huku akisisitiza kazi hiyo kuendelea katika maeneo mengine yenye changamoto kubwa.

Mwisho, Mwenyekiti huyo aliwataka madiwani, viongozi wa kata pamoja na wananchi kuendelea kushikamana na kushiriki kikamilifu katika kusimamia maendeleo ya halmashauri hiyo.

Ends..

Post a Comment

0 Comments