ARUSHA DC YAVUKA MALENGO YA MAKUSANYO YA MAPATO, MSUMI APONGEZA USHIRIKIANO WA MADIWANI NA WATAALAMU
Na Joseph Ngilisho| ARUMERU
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha (Arusha DC), Suleiman Msumi amesema halmashauri hiyo imefanikiwa kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato katika robo ya mwaka wa fedha unaoendelea, hatua aliyosema inaonesha namna ushirikiano kati ya madiwani, wataalamu na watendaji ulivyoendelea kuzaa matunda katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Msumi aliyasema hayo katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Arusha DC, ambapo alieleza kuwa hadi sasa halmashauri imefikisha asilimia 87 ya makusanyo ya mapato ya ndani huku lengo lililokuwa limewekwa kwa kipindi hicho likiwa ni asilimia 83.
Alisema mafanikio hayo yanatokana na usimamizi mzuri wa vyanzo vya mapato, ushirikiano wa madiwani pamoja na kazi kubwa inayofanywa na wataalamu wa halmashauri katika kuhakikisha huduma kwa wananchi zinaendelea kuimarika.
“Mpaka leo tunapozungumza tumesimamia asilimia 87 ya makusanyo ya mapato yetu kwa robo hii, ambapo kimsingi tulikuwa na lengo la asilimia 83. Hii inaonesha tumefanikiwa kuvuka malengo na tunaamini ifikapo mwisho wa mwaka wa fedha tutafikia asilimia mia moja,” alisema Msumi.
Mkurugenzi huyo alisema ndani ya kikao hicho madiwani walijadili masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwemo changamoto za barabara pamoja na matumizi ya Mfuko wa Jimbo, huku akisisitiza kuwa hoja zote zilizotolewa zitafanyiwa kazi kupitia kamati husika na vikao vya kisheria vya halmashauri.
Kwa niaba ya wataalamu wa Arusha DC, Msumi aliwashukuru madiwani kwa michango yao ya mawazo na ushauri unaoendelea kusaidia kuboresha utendaji wa halmashauri hiyo.
“Tumepata mawazo mapya na maelekezo mapya kutoka kwa waheshimiwa madiwani. Sisi kama wataalamu tunayapokea na tunaenda kuyafanyia kazi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wetu,” alisema.
Aidha, Msumi alisema halmashauri hiyo inaendelea kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia kwa kuboresha mifumo ya utendaji wa kazi kidijitali ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Katika hatua nyingine, aliipongeza Arusha DC kwa kuendelea kufanya vizuri kwenye masuala ya utumishi na michezo baada ya halmashauri hiyo kupata mafanikio mbalimbali katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika ngazi ya mkoa.
Alisema halmashauri ilifanikiwa kutwaa vikombe viwili katika mashindano mbalimbali huku zaidi ya watumishi 49 kutoka idara na vitengo tofauti wakitunukiwa zawadi kwa utendaji bora.
“Hatukupeleka bahasha tupu. Tulipeleka bahasha zenye fedha taslimu kwa ajili ya kuwapongeza watumishi wetu waliokuwa wamefanya vizuri katika maeneo yao ya kazi,” alisema.
Msumi aliongeza kuwa Arusha DC itaendelea kushirikiana na madiwani pamoja na viongozi wa kata katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ukusanyaji wa mapato na utoaji wa huduma bora kwa wananchi wa halmashauri hiyo.
Ends..









0 Comments