ARUSHA DC YAJIVUNIA MBUNGE MAKINI DKT LUKUMAY MATUMIZI YA FEDHA MFUKO WA JIMBO ,MADIWANI WAOMBA MGAWANYO SAWA

Na Joseph Ngilisho – ARUMERU


BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Arusha (Arusha DC) limetaka kuwepo kwa matumizi na mgawanyo wenye usawa wa fedha za Mfuko wa Mbunge ili kuhakikisha kata zote zinanufaika kwa uwiano sawa katika sekta za elimu, miundombinu ya barabara na huduma za jamii.

Katika kikao hicho, madiwani walisisitiza kuwa fedha hizo zinapaswa kusambazwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya kata badala ya kuonekana zikielekezwa zaidi kwenye maeneo machache, hatua ambayo kwa mujibu wao itasaidia kuharakisha maendeleo katika halmashauri nzima.

 

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arusha DC, Baraka Simion, aliunga mkono hoja hiyo akisema mgawanyo wa fedha hizo unapaswa kufanyika kwa haki na uwazi ili kila kata iweze kupata fursa ya kunufaika na miradi ya maendeleo inayotekelezwa kupitia Mfuko wa Mbunge.

Katika msisitizo wake, Mwenyekiti Baraka Simion alimuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri, Suleiman Msumi, kuhakikisha Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, anapatiwa mwaliko rasmi wa kushiriki vikao vya Baraza la Madiwani kama ilivyo kwa viongozi wengine wa kisheria.

Alisema mbunge huyo anastahili kushiriki moja kwa moja katika vikao hivyo kutokana na nafasi yake ya uwakilishi wa wananchi pamoja na mchango wake katika kusimamia miradi ya maendeleo kupitia Mfuko wa Jimbo, akibainisha kuwa uwepo wake utasaidia kuongeza ufanisi wa mijadala na kupata ufafanuzi wa moja kwa moja kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Suleiman Msumi alisema Mbunge Dkt. Lukumay yupo katika majukumu ya kibunge, lakini amekuwa na ushirikiano mzuri na halmashauri na kwamba taarifa zote za vikao hivyo anazipata kwa wakati, huku akipongeza usimamizi wake katika matumizi ya fedha za mfuko huo.

Baraza hilo pia lilijadili masuala mbalimbali ya maendeleo yakiwemo elimu, miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua, usalama wa wananchi pamoja na huduma za kijamii katika kata mbalimbali.

Katika mjadala huo, Diwani wa Kata ya Sokon II, Obedi Mollel, alihoji utaratibu wa mgawanyo wa fedha za Mfuko wa Mbunge akieleza kuwa kuna umuhimu wa kuhakikisha zinagawanywa kwa usawa ili kata zote ziweze kunufaika.

Hoja hiyo iliungwa mkono na madiwani wengine waliosisitiza uwiano katika ugawaji wa rasilimali hizo muhimu kwa maendeleo ya wananchi.

Katika kikao hicho pia, Mollel aliibua hoja ya kuipandisha hadhi Shule ya Sekondari Oldadai ili ianze kutoa elimu ya kidato cha tano na sita kutokana na ufaulu wake wa muda mrefu, ambapo Mkurugenzi Msumi alieleza kuwa kwa sasa kipaumbele ni kuongeza uwezo wa kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza kabla ya mchakato wa kidato cha tano na sita kuanza baadaye.

Mjadala mwingine ulihusu eneo la Kata ya Musa lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa chuo kikuu ambapo utekelezaji wake bado haujaanza, huku madiwani wakipendekeza wananchi waruhusiwe kulitumia kwa muda kwa shughuli za kilimo wakati wakisubiri mradi huo.

Kwa upande wa usalama, Diwani wa Enaboishu, Fauzia Mohamed, aliibua hoja kuhusu mnara wa mawasiliano uliopo Olturoto kukosa alama za tahadhari, ambapo Mkurugenzi Msumi aliahidi kushirikiana na TCRA pamoja na kampuni ya Yas kuhakikisha alama hizo zinawekwa.

Diwani wa Tarakwa, Abraham Lukumay, alihoji kuhusu changamoto za wageni wasio raia na upatikanaji wa huduma za NIDA, ambapo ilielezwa kuwa Serikali kupitia ofisi za Mkoa na Wilaya inaendelea kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.

Aidha, madiwani walijadili pia hatua ya kuipandisha hadhi Arusha DC kuwa mamlaka ya mji, ambapo Mkurugenzi alisema mchakato huo tayari umefikishwa ngazi za Mkoa kwa hatua zaidi za kiserikali.

Kuhusu miundombinu ya barabara, halmashauri ilieleza kuwa kwa kushirikiana na TARURA tayari imeanza matengenezo katika kata zote 27, huku zaidi ya shilingi bilioni mbili zikitengwa kwa kazi hiyo.

Mwenyekiti Baraka Simion alisisitiza pia umuhimu wa kujenga mifereji na miundombinu bora ya maji ya mvua ili kulinda barabara dhidi ya uharibifu unaojitokeza mara kwa mara.









Post a Comment

0 Comments