ASKARI SABA MBARONI KWA KUMUUA MWALIMU KWA RISASI

 ASKARI SABA WA TAWA WAKAMATWA KUHUSIANA NA KIFO CHA MWALIMU KATAVI

Arushadigital|KATAVI




Jeshi la Polisi mkoani Katavi linawashikilia askari saba wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa tuhuma za kuhusika na kifo cha mwalimu wa Shule ya Msingi Kamsisi, Une Mwakabange (42), aliyefariki dunia baada ya kupigwa risasi wakati wa operesheni ya doria ndani ya Pori la Inyonga wilayani Mlele.

Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, tukio hilo lilitokea Mei 6 mwaka huu wakati askari hao wa TAWA walipokuwa wakifanya doria katika eneo hilo la hifadhi. Inadaiwa kuwa askari hao waliwaona watu watatu wakiwa na pikipiki na kuanza kuwafukuza wakihisi kuwa ni watu wenye shughuli zisizo halali ndani ya pori hilo.

Katika harakati za msako huo, askari mmoja aliyetajwa kwa jina la James Daniel (25), anadaiwa kufyatua risasi iliyompiga Une Mwakabange mguuni na kusababisha aanguke chini akiwa katika hali mbaya.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mwalimu huyo alikimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu, hata hivyo alifariki dunia njiani kutokana na majeraha aliyoyapata.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini mazingira halisi ya tukio hilo pamoja na kuwawajibisha wote watakaobainika kuhusika na kifo hicho.

Ends..


Post a Comment

0 Comments