MEYA WA JIJI LA ARUSHA AJIVUNIA MIRADI YA MAENDELEO YA BILIONI 39.58

 MEYA WA JIJI LA ARUSHA AJIVUNIA MIRADI YA MAENDELEO YA BILIONI 39.58

Na Joseph Ngilisho|ARUSHA

MEYA  wa Jiji la Arusha, Maximilian Iranghe amesema Jiji la Arusha linaendelea kupiga hatua kubwa za maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 39.58 inayotekelezwa katika kata zote 25 za jiji hilo.


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, May 9,2026, Meya Iranghe alisema miradi hiyo inalenga kuboresha huduma za kijamii, miundombinu pamoja na kuifanya Arusha kuwa jiji la kisasa linalokidhi hadhi yake kama kitovu cha utalii na makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Alisema katika robo ya tatu na robo ya mwisho ya mwaka wa fedha 2025/2026, halmashauri hiyo imesaini na kuanza utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Polisi katika Kata ya Moshono wenye thamani ya shilingi milioni 145.9 pamoja na ujenzi wa mtaro wa Suye wenye gharama ya shilingi milioni 100.2.


Aidha, alisema jiji hilo linaendelea na ujenzi wa vifuko viwili katika Kata ya Muriet kwa gharama ya shilingi milioni 64.5 huku magari mawili aina ya Toyota Pick Up yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 363 tayari yakiwa yamepokelewa kwa ajili ya kuimarisha shughuli za utoaji huduma.


Katika sekta ya elimu, Meya huyo alisema halmashauri inaendelea na ujenzi wa jengo la Shule ya Sekondari Bondeni City kwa gharama ya shilingi milioni 760 pamoja na ujenzi wa Shule ya Msingi Ungalimited unaogharimu shilingi milioni 877.


Pia alisema madarasa manne na ofisi mbili zinajengwa katika Shule ya Msingi Osunya kwa gharama ya shilingi milioni 636 huku ukarabati wa ofisi za Halmashauri ya Jiji la Arusha ukiendelea kwa zaidi ya shilingi milioni 903.


Meya Iranghe alisema sekta ya afya nayo imepewa kipaumbele ambapo jiji hilo linaendelea na ujenzi wa jengo la OPD katika Hospitali ya Wilaya kwa gharama ya shilingi bilioni 11.25 ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi.


Aliongeza kuwa ujenzi wa Shule ya Msingi Muriet wenye thamani ya shilingi milioni 771 nao unaendelea sambamba na mradi mkubwa wa jengo jipya la utawala la ghorofa unaogharimu shilingi bilioni 9.3.


Kwa mujibu wa Meya huyo, jengo hilo litakuwa miongoni mwa majengo ya kisasa na marefu zaidi yanayomilikiwa na halmashauri nchini likiwa na kumbi za mikutano, migahawa pamoja na huduma nyingine muhimu za kijamii na kiutawala.


Katika hatua nyingine, Meya Iranghe alisema Jiji la Arusha limeendelea kufanya vizuri katika suala la usafi wa mazingira baada ya kuibuka kinara kitaifa miongoni mwa majiji yote nchini Tanzania.


Kutokana na mafanikio hayo, alisema halmashauri imenunua bulldozer kwa ajili ya kuboresha dampo la Muriet ili kuendelea kuimarisha usimamizi wa taka na mazingira ya jiji hilo.


Aidha, alisema jiji hilo linaendelea na ujenzi wa Barabara ya Giriki ambayo itakuwa ya kwanza Arusha kujengwa kwa mfumo wa zege badala ya lami ya kawaida.


Mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 1.27 unahusisha ujenzi wa kilomita 1.21 za barabara pamoja na mifereji ya maji ya mvua na vifuko.


Sambamba na hilo, box culvert kubwa zinaendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kata ya Kaloleni, Lemara na Olorien kwa gharama ya mamia ya mamilioni ya shilingi ili kukabiliana na changamoto ya miundombinu ya maji ya mvua.


Meya Iranghe alisema miradi hiyo yote ni sehemu ya dhamira ya kulifanya Jiji la Arusha kuwa jiji la kisasa, salama na lenye miundombinu bora inayovutia uwekezaji, utalii pamoja na shughuli za kidiplomasia katika ukanda wa Afrika Mashariki.


Ends..

Post a Comment

0 Comments