SERIKALI YAAHIDI KUTATUA CHANGAMOTO ZA WAUGUZI, TANNA YALILIA MUUNDO MPYA WA UTUMISHI

SERIKALI YAAHIDI KUTATUA CHANGAMOTO ZA WAUGUZI, TANNA YALILIA MUUNDO MPYA WA UTUMISHI

 Na Joseph Ngilisho |ARUSHA 

SERIKALI imewahakikishia wauguzi na wakunga nchini kuwa itaendelea kushughulikia changamoto zao za kiutumishi, kuboresha mazingira ya kazi pamoja na kuhakikisha kunakuwa na fursa sawa za uongozi katika sekta ya afya bila kuangalia taaluma moja pekee.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa kupitia hotuba yake iliyosomwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Toba Nguvila, wakati wa Kongamano la Kisayansi na Mkutano Mkuu wa 55 wa Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA) uliofanyika jijini Arusha Mei 9, 2025.

Katika hotuba hiyo, Waziri Mchengerwa alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya kupitia ujenzi wa miundombinu, ununuzi wa vifaa tiba, kuongeza ajira pamoja na kuwajengea uwezo wauguzi na wataalamu wengine wa afya.

Alisema wauguzi ni mhimili mkubwa wa utoaji huduma za afya nchini kwani wanaunda zaidi ya asilimia 60 ya watumishi wote wa sekta hiyo huku wakitekeleza zaidi ya asilimia 80 ya shughuli za afya.


“Bila wauguzi huduma za afya zitayumba. Serikali inatambua mchango wao mkubwa katika kulinda afya za wananchi na itaendelea kuboresha maslahi yao kadri hali ya uchumi itakavyozidi kuimarika,” alisema.

Aidha, alisema Serikali tayari imeanza kushughulikia changamoto ya muundo wa utumishi kwa kada ya uuguzi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, huku mapendekezo mbalimbali yakiwa tayari yamefanyiwa kazi.

Kuhusu malalamiko ya wauguzi juu ya nafasi za uongozi katika sekta ya afya, Waziri Mchengerwa alisema uongozi haupaswi kuangalia taaluma moja pekee bali uzingatie uwezo wa kiuongozi, elimu, uzoefu, uadilifu na uzalendo.

“Nawaelekeza watendaji wangu kuhakikisha mapitio ya sheria na sera husika yanafanyika ili kutoa fursa sawa za uongozi kwenye sekta ya afya,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo aliipongeza TANNA kwa maandalizi mazuri ya kongamano hilo pamoja na utoaji wa huduma za afya bure kwa wananchi, akisema hatua hiyo inaongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa taaluma ya uuguzi.

Pia aligusia kauli mbiu ya Siku ya Wauguzi Duniani ya mwaka 2025 isemayo “Wauguzi Wetu, Mustakabali Wetu, Wauguzi Waliowezeshwa Huokoa Maisha”, akisema ujumbe huo unaonesha umuhimu wa kuwathamini wauguzi kutokana na mchango wao mkubwa katika kuokoa maisha ya wananchi.

Aliwataka wauguzi kuendelea kufanya kazi kwa weledi, huruma, upendo na moyo wa kujitolea huku akisisitiza kuwa huduma zenye utu na maneno mazuri kwa wagonjwa ni sehemu muhimu ya tiba.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha,Jacob Rombo alisema Serikali imeendelea kuimarisha sekta ya afya kupitia uwekezaji mkubwa wa miundombinu, vifaa tiba pamoja na kuongeza wataalamu wa afya.

Alisema kongamano hilo limekuwa jukwaa muhimu la kujadili changamoto zinazowakabili wauguzi pamoja na kuja na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha huduma za afya nchini.

“Maadhimisho haya yanatupa nafasi ya kutambua mchango mkubwa wa wauguzi katika kuokoa maisha ya wananchi. Serikali inatambua kazi kubwa mnayoifanya na itaendelea kuwaunga mkono,” alisema.

CPA Makalla alisema kati ya mwaka 2022 hadi 2026 zaidi ya shilingi bilioni 3.8 zimetumika kuboresha mifumo ya utoaji huduma za afya mkoani Arusha huku zaidi ya shilingi bilioni 34.5 zikielekezwa katika ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa pamoja na ujenzi wa miundombinu ya afya.

Aidha, alisema zaidi ya shilingi bilioni 63.38 zimetumika mkoani humo kati ya mwaka 2021 hadi 2025 kwa ajili ya kuimarisha sekta ya afya, hali iliyosaidia kuongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kutoka asilimia 95 hadi 99.

Alibainisha kuwa Serikali inaendelea kuimarisha rasilimali watu katika sekta ya afya kwa kuajiri watumishi wapya wakiwemo wauguzi ili kupunguza upungufu wa wataalamu katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Hata hivyo, Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA) kimeiomba Serikali kuharakisha utekelezaji wa muundo mpya wa utumishi kwa kada ya uuguzi na ukunga, kikisema kuchelewa kwa maboresho hayo kumeendelea kushusha morali ya watumishi na kuathiri utoaji wa huduma bora za afya.

Katika risala iliyosomwa na Katibu wa TANNA, Dkt. Godfrey Chacha, chama hicho kilisema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya, wauguzi na wakunga bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazodhoofisha mazingira ya kazi.

TANNA ilieleza kuwa wauguzi na wakunga ni zaidi ya asilimia 75 ya watumishi wote wa sekta ya afya nchini, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kuwekeza katika ustawi wa kada hiyo ambayo ndiyo uti wa mgongo wa huduma za afya.

Dkt. Chacha alisema TANNA imeendelea kutoa mafunzo endelevu ya kitaaluma (CPD), kushiriki makongamano ya kimataifa pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma na nchi mbalimbali ikiwemo Malawi, Zimbabwe na Rwanda kwa lengo la kuboresha huduma za afya nchini.

Aidha, alisema chama hicho kimeendelea kutoa tuzo za kutambua utendaji bora kwa wauguzi na wakunga pamoja na kushiriki katika shughuli za kijamii zikiwemo kampeni za uchangiaji damu, elimu ya afya na utoaji wa huduma za uuguzi kwa jamii.

Hata hivyo, TANNA ilieleza kusikitishwa na kuchelewa kwa utekelezaji wa muundo mpya wa utumishi ambao ulianza kujadiliwa tangu mwaka 2013 lakini hadi sasa haujatekelezwa.

Kwa mujibu wa chama hicho, muundo wa sasa hautambui ipasavyo maendeleo ya taaluma kwa wauguzi wenye shahada, shahada za uzamili pamoja na ubobezi mbalimbali jambo linalopunguza motisha kwa watumishi wengi kujiendeleza kielimu

“Muundo mpya wa utumishi utasaidia kuongeza motisha kwa wauguzi na wakunga kujiendeleza kitaaluma hadi kufikia ngazi za ubingwa na ubingwa bobezi, jambo litakaloongeza tija na ubora wa huduma za afya nchini,” alisema Dkt. Chacha.

Pia TANNA ilieleza kuwepo kwa changamoto katika mfumo wa utawala ndani ya sekta ya afya ambapo nafasi nyingi za kiutawala zimekuwa zikitolewa zaidi kwa kada moja pekee huku kada nyingine muhimu kama uuguzi na ukunga zikikosa uwakilishi wa kutosha katika ngazi za maamuzi.

Kutokana na hali hiyo, chama hicho kiliitaka Serikali kufanya maboresho ya kiutawala yatakayotoa nafasi sawa kwa kada zote za afya ili kuongeza ufanisi wa huduma pamoja na kuimarisha ushirikiano katika sekta hiyo.

Mkutano huo wa 55 wa TANNA umewakutanisha wauguzi, wakunga, wataalamu wa afya na wadau mbalimbali kutoka maeneo tofauti nchini kujadili maendeleo ya taaluma ya uuguzi pamoja na changamoto zinazoikabili sekta ya afya nchini.

Ends..

Post a Comment

0 Comments