LATIFA AKUTWA AMEFARIKI LODGE ARUSHA, PESA NA SIMU VYADAIWA KUIBIWA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
MWANAMKE aliyefahamika kwa jina moja la Latifa, anayedaiwa kujishughulisha na biashara ya ngono, amefariki dunia katika mazingira ya kutatanisha baada ya kukutwa ndani ya chumba cha kulala wageni katika Lodge ya Dolphin, eneo la Kaloleni jijini Arusha.
Tukio hilo linadaiwa kutokea usiku wa kuamkia Oktoba 18, 2026, ambapo marehemu alikutwa ndani ya chumba namba nne akiwa na mikono iliyofungwa, mdomo uliozibwa na mtandio uliokuwa umefungwa shingoni huku akiwa uchi wa mnyama akiwa ametumika
Kwa mujibu wa mashuhuda, Latifa alikuwa amepangisha chumba hicho kwa Sh30,000 tangu mchana, kabla ya kuingia ndani akiwa na mwanaume anayedaiwa kuwa mteja wake.
Baada ya kuona amekaa muda mrefu bila kutoka, marafiki zake waliamua kwenda kumuangalia, ndipo walipomkuta katika hali hiyo na kumkimbiza Hospitali ya Mount Meru kwa ajili ya matibabu.
Hata hivyo, walipofika hospitalini hapo, walibaini kuwa tayari alikuwa amefariki dunia.
Aidha, mwanaume anayedaiwa kuingia na marehemu chumbani hapo anadaiwa kuondoka na fedha pamoja na simu ya Latifa, ingawa taarifa hizo bado zinahitaji kuthibitishwa na vyombo vya uchunguzi.
Hadi sasa, utambulisho wa mwanaume huyo na chanzo rasmi cha kifo cha Latifa havijawekwa wazi.
Tukio hilo linahitaji uchunguzi wa kina wa vyombo vya dola ili kubaini chanzo cha kifo, mazingira yaliyopelekea marehemu kufariki na ukweli wa madai ya kuibiwa kwa mali zake.
Ends

Post a Comment