NDEJEMBI ACHARUKIA UZEMBE TANROADS, AAGIZA HATUA
Na Joseph Ngilisho | MBEY
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amekerwa na uzembe na taarifa zisizo sahihi alizodai kutolewa na Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Suleiman Bishanga, kuhusu ufunguaji wa barabara ya njia nne katika eneo la Mdope.
Ndejembi ametoa kauli hiyo baada ya kurejea kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika eneo la Kabwe, akitaka hatua zichukuliwe kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi ili kupunguza adha kwa watumiaji wa barabara hiyo.
Amehoji sababu za Serikali kutumia Sh bilioni 40 katika mradi huo bila kuona matokeo yanayolingana na fedha zilizotumika, akisisitiza kuwa kiasi hicho ni kikubwa na hakipaswi kuambatana na uzembe au usimamizi dhaifu.
Kutokana na hali hiyo, Makamu wa Rais amemtaka Waziri wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, kuhakikisha hatua za uwajibikaji zinachukuliwa dhidi ya watendaji watakaobainika kutoa taarifa zisizo sahihi na kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Amesisitiza kuwa Serikali haitavumilia watendaji wanaopotosha taarifa za utekelezaji wa miradi ya umma huku wananchi wakiendelea kukabiliwa na changamoto za miundombinu.
Ends


Post a Comment