ARUSHA DC YAANZA KUREKEBISHA BARABARA KOROFI ZILIZOHARIBIWA NA MVUA, ZAIDI YA BILIONI 2 KUTUMIKA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Halmashauri ya Wilaya ya Arusha (Arusha DC) imeanza rasmi zoezi la kuzifanyia matengenezo barabara zilizoharibiwa vibaya na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, huku barabara ya Korofi eneo la Sekei karibu na ofisi za halmashauri hiyo ikiwa miongoni mwa zilizoanza kufanyiwa kazi kwa haraka.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya wananchi kulalamikia ubovu mkubwa wa barabara hiyo ambao ulikuwa unasababisha usumbufu kwa watumiaji wa vyombo vya usafiri pamoja na wakazi wa maeneo hayo, hasa kipindi cha mvua.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Arusha DC, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Suleiman Msumi, amesema tayari maagizo ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mheshimiwa Ahmed Mwinyi, yameanza kutekelezwa kwa vitendo ambapo kazi za matengenezo zimeanza rasmi.
Msumi amesema kwa sasa greda limeanza kazi ya kusawazisha barabara hiyo huku zaidi ya tani 150 za vifusi zikiendelea kuwekwa ili kuboresha hali ya upitishaji magari na wananchi.
“Tumeshanza kazi rasmi. Greda linaendelea na usawazishaji wa barabara na tunaendelea kuweka vifusi kwa lengo la kuhakikisha eneo hili linapitika wakati wote hata kipindi cha mvua,” amesema Msumi.
Ameeleza kuwa matengenezo hayo yataanzia eneo la Sekei karibu na Halmashauri ya Arusha DC hadi mwisho wa Shule ya Ngeresi, huku mkazo mkubwa ukiwekwa katika kuboresha mfumo wa maji ya mvua ili kuzuia barabara kuendelea kuharibika mara kwa mara.
Kwa mujibu wa Msumi, pamoja na hatua za sasa za dharura, barabara hiyo tayari imeingizwa katika mpango wa maendeleo wa mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami.
Amesema kazi zinazofanyika kwa sasa zinatekelezwa kwa ushirikiano wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), ambao wanaendelea na uwekaji wa kifusi pamoja na maboresho ya mifereji na miundombinu ya kupitisha maji.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arusha DC, Baraka Simion, amesema TARURA imetenga zaidi ya shilingi bilioni mbili kwa ajili ya ukarabati wa barabara katika kata zote 27 za halmashauri hiyo ambazo nyingi zimeathiriwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
Amesema fedha hizo zitaelekezwa katika kurejesha mawasiliano ya barabara yaliyoharibika ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao za kijamii na kiuchumi bila changamoto kubwa za usafiri.
“Barabara nyingi zimeharibika kutokana na mvua kubwa, lakini tayari serikali kupitia TARURA imetenga fedha za kutosha kuhakikisha matengenezo yanafanyika katika kata zote,” amesema Simion.
Aidha, Mkurugenzi Msumi aliwahakikishia madiwani kuwa serikali inaendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa changamoto ya miundombinu ya barabara katika Arusha DC.
Amesema Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mheshimiwa Ahmed Mwinyi, tayari ameenda Dodoma kwa ajili ya mazungumzo na Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega, kuomba fedha za dharura zitakazosaidia kuboresha zaidi hali ya barabara zilizoathiriwa na mvua.
Hatua hiyo imepokelewa kwa matumaini makubwa na wananchi wa Arusha DC ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikumbana na changamoto za usafiri kutokana na ubovu wa baadhi ya barabara za ndani, hasa kipindi cha mvua kubwa.

0 Comments