DIWANI MREMA AITAKA ARUSHA DC KUWEKEZA ZAIDI KWENYE MICHEZO KUPUNGUZA UHALIFU

 DIWANI MREMA AITAKA ARUSHA DC KUWEKEZA ZAIDI KWENYE MICHEZO KUPUNGUZA UHALIFU

Na Joseph Ngilisho-ARUSHA 

Diwani wa Kata ya Mlangarini, Emanuel Mrema, ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha DC kuweka mkazo zaidi katika maendeleo ya michezo akisema ni nyenzo muhimu ya kuunganisha jamii na kupunguza vitendo vya uhalifu miongoni mwa vijana.

Mrema alitoa kauli hiyo Leo May 8,2026 wakati akichangia hoja katika Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Arusha DC lililofanyika Wilayani Arumeru, ambapo alisema baadhi ya maeneo bado hayana mazingira rafiki ya kukuza michezo licha ya umuhimu wake kwa jamii.


Alisema kwa sasa maeneo ambayo michezo imeanza kuonekana kwa kiwango fulani ndani ya Mji wa Mlangarini ni Olomiti na Kitenge, huku maeneo mengine yakikosa kabisa miundombinu na programu za michezo zinazoweza kuwashirikisha vijana.

“Michezo ni sehemu muhimu sana ya kuunganisha jamii lakini pia ni njia bora ya kupunguza uhalifu katika maeneo yetu. Tukiviinua vikundi vya michezo tutasaidia vijana kupata sehemu sahihi ya kutumia muda wao na kujenga mshikamano wa kijamii,” alisema Mrema.

Aidha, aliitaka Kamati husika ndani ya Halmashauri hiyo kuandaa mpango maalum wa kusaidia na kuviwezesha vikundi vya michezo ili viweze kuwa chachu ya maendeleo kwa vijana pamoja na kuongeza manufaa kwa Halmashauri kupitia shughuli za kijamii na kiuchumi.

Kauli ya Diwani huyo imekuja wakati serikali na wadau mbalimbali wakiendelea kusisitiza umuhimu wa michezo kama sehemu ya kukuza vipaji, ajira kwa vijana na njia ya kupambana na mmomonyoko wa maadili katika jamii.



Ends .

Post a Comment

0 Comments