UHURU WA VYOMBO VYA HABARI WAZIDI KUPOROMOKA – DKT. ANNA HENGA AONYA

 UHURU WA VYOMBO VYA HABARI WAZIDI KUPOROMOKA – DKT. ANNA HENGA AONYA

Na Joseph Ngilisho| ARUSHA

MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Anna Henga, amesema hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchini imeendelea kudorora kwa kiwango kikubwa, akibainisha kuwa mwenendo huo ulijitokeza zaidi mwaka uliopita na unaendelea kushuhudiwa hata mwaka huu.

Dkt. Henga alitoa kauli hiyo leo April 29,2026 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yanayofanyika jijini Arusha, ambapo wadau wa sekta ya habari walikutana kujadili hali ya uhuru wa vyombo vya habari na mustakabali wake nchini.

Akizungumzia tathmini ya haki za binadamu inayochambua takriban haki 60 kila mwaka—ikiwemo haki za kisiasa na kiraia, haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni pamoja na haki za makundi maalum—alisema sekta ya habari imeendelea kuwa miongoni mwa zilizoathirika zaidi.

Alieleza kuwa mwaka uliopita, uliokuwa na muktadha wa uchaguzi, uliambatana na matukio mengi yaliyoathiri moja kwa moja wanahabari, yakiwemo kukamatwa kwa baadhi yao, kupotea katika mazingira ya kutatanisha na hata matukio ya mauaji.

“Katika kipindi hicho tulishuhudia wanahabari kadhaa wakikamatwa kinyume cha taratibu, wengine kupotea na baadhi kuuawa. Haya yote yanaashiria mazingira magumu kwa uhuru wa habari,” alisema.

Kwa mujibu wa Dkt. Henga, takriban wanahabari wanane walikamatwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Musoma, Dar es Salaam na Arusha, huku baadhi yao wakishikiliwa bila kufikishwa mahakamani, hali inayokiuka misingi ya haki.

Aidha, alitaja kufungwa kwa huduma za intaneti hasa wakati wa uchaguzi kuwa kikwazo kikubwa kwa vyombo vya habari vya mtandaoni, akisema hatua hiyo ilidhoofisha upatikanaji wa taarifa kwa wananchi.

“Unapofunga intaneti, unazima kabisa uwezo wa vyombo vya habari kufanya kazi. Hili ni pigo kubwa kwa uhuru wa habari katika zama za kidijitali,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa vyombo kadhaa vya habari vilifungiwa kwa nyakati tofauti, hali iliyodhoofisha tasnia hiyo, huku akibainisha kuwa hata katika robo ya kwanza ya mwaka huu, matukio ya kufungiwa kwa vyombo na kukamatwa kwa wanahabari yameendelea kuripotiwa.

Akizungumzia ubunifu wa wanahabari, Dkt. Henga alisema hauwezi kukua katika mazingira yenye hofu na vikwazo.

“Mwanahabari hawezi kuwa mbunifu kama hana uhuru. Lazima kuwe na mazingira salama na huru ili aweze kufanya kazi yake kwa ufanisi,” alisema.

Kuhusu mfumo wa kisheria, alieleza kuwa licha ya Katiba ya Tanzania, hususan Ibara ya 18 kulinda uhuru wa kutoa na kusambaza taarifa, bado kuna changamoto katika sheria za maudhui na sheria za habari ambazo hazitoi uhuru wa kutosha kwa wanahabari.

Alisisitiza umuhimu wa kufuata misingi ya haki (due process) pale ambapo mwanahabari au chombo cha habari kinapotuhumiwa kukiuka sheria, badala ya kuchukua hatua za haraka kama kufungia bila kusikilizwa.

“Ni muhimu kuhakikisha kuwa kuna utaratibu wa haki unaofuatwa. Mwanahabari apewe nafasi ya kusikilizwa kabla ya kuchukuliwa hatua yoyote,” alieleza.

Akizungumzia mahusiano kati ya serikali na vyombo vya habari, Dkt. Henga alisema bado yana mvutano, huku serikali ikiviona vyombo vya habari kama wakosoaji badala ya washirika wa uwazi na uwajibikaji.

Alishauri serikali kuviona vyombo vya habari kama chombo cha kujitathmini na siyo adui, akisisitiza kuwa ukosoaji ni sehemu muhimu ya utawala bora.

Katika hatua nyingine, aligusia kesi za kimkakati zilizofunguliwa kupinga baadhi ya vifungu vya sheria vinavyodaiwa kukandamiza uhuru wa habari, akieleza kuwa licha ya baadhi ya maamuzi ya mahakama kuwa na mwelekeo chanya, utekelezaji wake bado ni changamoto.

Kwa ujumla, Dkt. Henga alitoa wito kwa serikali kufanya maboresho ya kisheria na kiutendaji ili kulinda uhuru wa vyombo vya habari, akionya kuwa bila hatua madhubuti, hali inaweza kuendelea kudhoofika na kuathiri demokrasia pamoja na haki ya wananchi kupata taarifa sahihi kwa wakati.

Katika maadhimisho ya mwaka huu yaliyofanyika jijini Arusha, wadau mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari, wahariri, wanazuoni, wanaharakati wa haki za binadamu na wawakilishi wa serikali wamekutana kujadili nafasi ya vyombo vya habari katika kukuza demokrasia, uwazi na maendeleo endelevu.

Kaulimbiu ya mwaka huu imelenga kuhimiza uadilifu wa habari katika enzi ya kidijitali, huku ikisisitiza umuhimu wa kupambana na changamoto ya taarifa potofu na matumizi mabaya ya majukwaa ya kidijitali yanayoendelea kuathiri uaminifu wa taarifa kwa jamii.

Post a Comment

0 Comments