LHRC YAKUNJUA MAKUCHA YATAKA MAREKEBISHO YA KANUNI ZA MTANDAONI KULINDA UHURU WA HABARI

LHRC YAKUNJUA MAKUCHA YATAKA MAREKEBISHO YA KANUNI ZA MTANDAONI KULINDA UHURU WA HABARI

Na Joseph Ngilisho| ARUSHA DIGITAL 

ARUSHA — Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetoa wito kwa Serikali kufanya marekebisho ya haraka ya kanuni za maudhui mtandaoni ili kulinda haki ya msingi ya kusikilizwa na kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari nchini yanayofanyika jijini Arusha,loe April 29,2026 Meneja wa Uchechemuzi wa LHRC, Raymond Paul Kanegene, alisema kuwa taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa mstari wa mbele kufungua kesi za kimkakati katika mahakama za ndani na za kimataifa ili kuhakikisha haki za kikatiba, ikiwemo uhuru wa kujieleza na habari, zinalindwa.

Alieleza kuwa miongoni mwa kesi hizo ni ile iliyofunguliwa katika Mahakama ya Afrika Mashariki pamoja na mahakama za ndani kupinga baadhi ya vipengele vya Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni za mwaka 2020 na 2022.

Kwa mujibu wa Kanegene, kesi hiyo ilifunguliwa na Deus Valentin Raymond kwa lengo la kupinga vifungu vinavyokiuka haki za msingi, hususan haki ya kusikilizwa kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria au kiutawala.

“Mahakama ya Rufaa, ambayo ni chombo cha juu kabisa cha utoaji haki nchini, ilitoa uamuzi Desemba 25, 2020 ikibainisha kuwa Kifungu cha 8 cha kanuni hizo ni batili kwa kuwa kinakiuka Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.

Alifafanua kuwa kifungu hicho kinashindwa kutoa haki kwa mtu anayetuhumiwa mbele ya Kamati ya Maudhui ya Mtandaoni kwa kutompa nafasi ya kusikilizwa au kujitetea kabla ya kuchukuliwa hatua.

“Ni kanuni ya msingi ya haki kwamba hakuna mtu anayepaswa kuhukumiwa au kuadhibiwa bila kupewa nafasi ya kusikilizwa. Lakini kifungu hiki kinakwenda kinyume na misingi hiyo,” alisisitiza.

Kanegene aliongeza kuwa licha ya uamuzi huo wa mahakama, bado kanuni hiyo haijafanyiwa marekebisho, hali inayochangia kuendelea kwa malalamiko kutoka kwa wadau wa vyombo vya habari kuhusu hatua za kufungiwa au kusimamishwa bila kusikilizwa.

Kutokana na hali hiyo, LHRC imetoa wito kwa Serikali kuzingatia maamuzi ya mahakama na kufanya marekebisho ya haraka ya kanuni hizo ili kuhakikisha haki za msingi, hususan haki ya kusikilizwa, zinaheshimiwa na kulindwa.

“Ni muhimu sasa Serikali ichukue hatua za makusudi kurekebisha kifungu hicho ili kuendana na matakwa ya Katiba na viwango vya haki za binadamu vya kimataifa,” alihitimisha.

Ends..

Post a Comment

0 Comments