BABA AMCHINJA MTOTO WAKE WA MIEZI 8 ARUSHA
Na Joseph Ngilisho| ARUSHA
SIMANZI, hofu na hasira vimetawala wakazi wa eneo la Sinoni jijini Arusha kufuatia tukio la kikatili la kuuawa kwa mtoto wa miezi nane, Sahiri Salmin, anayedaiwa kuchinjwa na baba yake mzazi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha iliyotolewa Aprili 28, 2026, mtuhumiwa wa tukio hilo ametajwa kuwa ni Salmin Rajabu (29), fundi ujenzi na mkazi wa eneo hilo, ambaye anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kutekeleza mauaji hayo ya kinyama.
Inaelezwa kuwa tukio hilo lilitokea jioni katika makazi ya familia hiyo, wakati mama wa mtoto alipokuwa ametoka kwenda dukani kununua tambi akiwa ameongozana na mtoto wao mkubwa, hali iliyomwacha marehemu akiwa nyumbani na baba yake.
Mashuhuda wa tukio hilo wanasema awali hawakutilia shaka kelele za mtoto zilizokuwa zikisikika, wakidhani ni watoto wanaocheza.
Hata hivyo, hali ilibadilika ghafla pale jirani mmoja alipokwenda kuchungulia na kukuta mwili wa mtoto ukiwa umetenganishwa kichwa na kiwiliwili, ukiwa umelala sakafuni huku damu nyingi ikivuja.
“Tulishtuka sana. Tulidhani ni kelele za kawaida za watoto, lakini tulipofika ndani tukakuta hali ya kutisha sana,” alisimulia mmoja wa majirani kwa sharti la kutotajwa jina.
Mashuhuda wengine walidai kuwa mama aliporudi nyumbani alikuta mlango umefungwa kwa ndani, na baada ya kusubiri kwa muda, mtuhumiwa alifungua mlango akiwa amepiga magoti na kukiri kutekeleza tukio hilo.
Taarifa za tukio hilo ziliposambaa, wananchi wenye hasira walijaribu kumshambulia mtuhumiwa kwa lengo la kujichukulia sheria mkononi, lakini askari wa Jeshi la Polisi waliwasili kwa haraka na kufanikiwa kumuokoa kabla ya kupelekwa kituoni kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Aidha, polisi walichukua mwili wa mtoto huyo na kuupeleka katika kituo cha afya kwa ajili ya uchunguzi na taratibu nyingine za kisheria.
Tukio hilo limeibua maswali mazito miongoni mwa wakazi wa eneo hilo, huku baadhi wakidai kuwa mtuhumiwa alikuwa na changamoto ya afya ya akili, ingawa madai hayo bado hayajathibitishwa rasmi na vyombo vya dola.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Justine Masejo, alisema uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha tukio hilo na hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa.
Jeshi la Polisi limewataka wananchi kutulia na kuacha kujichukulia sheria mkononi, likisisitiza kuwa haki itatendeka kwa mujibu wa sheria baada ya kukamilika kwa uchunguzi.
Tukio hili limeacha majonzi makubwa kwa familia, majirani na jamii kwa ujumla, huku likikumbusha umuhimu wa uangalizi wa afya ya akili na mshikamano wa kijamii katika kuzuia matukio ya aina hii.
ENDS..

0 Comments