WAZIRI HOMERA ASISITIZA UTAWALA BORA, MABORESHO YA SHERIA KUIMARISHA UFANISI WA TAASISI ZA SERIKALI,AG ASISITIZA SERIKALI KUBORESHA MIFUMO YA UTENDAJI KAZI

 WAZIRI HOMERA ASISITIZA UTAWALA BORA, MABORESHO YA SHERIA KUIMARISHA UFANISI WA TAASISI ZA SERIKALI

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kisheria nchini, akibainisha kuwa maboresho ya mifumo ya sheria ni nyenzo muhimu katika kuharakisha maendeleo ya taifa na kuimarisha utendaji wa taasisi za umma.

Akifungua Mkutano wa Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) April 28,2026 jijini Arusha, Dkt. Homera amesema Serikali itaendelea kuboresha mifumo ya kisheria na taasisi zake ili ziendane na kasi ya mabadiliko ya kiuchumi na kijamii, huku akisisitiza kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ina nafasi ya kipekee katika kulinda misingi ya haki na maslahi ya taifa.

Amesema watumishi wa ofisi hiyo wanapaswa kuwa nguzo muhimu ya ushauri wa kisheria serikalini kwa kuzingatia weledi, nidhamu na uadilifu katika utendaji wao wa kazi.

“Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni mhimili muhimu katika kuhakikisha Serikali inafanya maamuzi yake kwa mujibu wa sheria. Ni lazima muendelee kuwa makini, wenye weledi na wanaozingatia maslahi mapana ya taifa,” amesema Dkt. Homera.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali za serikali katika kuharakisha mabadiliko ya kisheria alisisitiza kuwa serikali kupitia mwanasheria mkuu, serikali ipo mbioni kuibadili sheria 1000 ikilenga kuboresha mazingira ya uwekezaji, kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi na kuimarisha utendaji wa taasisi za umma.

Katika hotuba yake, Waziri Homera pia amesema kuwa Serikali iko mbioni kufanya maboresho ya sheria mbalimbali ili ziende sambamba na malengo ya Dira Taifa 2050.

Amewahimiza watumishi kuendelea kujifunza na kujiendeleza kitaaluma ili kuendana na mabadiliko ya dunia ya sasa na kufikia dira ya Taifa ya 2050, akibainisha kuwa ujuzi na maarifa ni msingi wa utoaji wa huduma bora na tija kazini.

Amehitimisha kwa kuwataka watumishi hao kuwa mfano wa uadilifu na uzalendo katika utumishi wa umma, huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika kuboresha mazingira ya kazi ili kuongeza ufanisi.

Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, amewataka watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufanya kazi kwa mshikamano, nidhamu na kujituma ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za kisheria kwa umma.

Katika mkutano huo, Johari amesema kuwa ili kufikia malengo ya Dira 2050 ni muhimu kwa Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakaongeza kasi katika maboresho ya Sheria mbalimbali

 Amesema mafanikio ya taasisi hayategemei mtu mmoja bali ni matokeo ya juhudi za pamoja za watumishi wote bila kujali nafasi zao.

Alisisitiza kuwa ofisi hiyo inapaswa kujengwa katika misingi ya “timu moja, lengo moja,” akibainisha kuwa hakuna nafasi ya kufanya kazi kwa mazoea au kujiona bora kuliko wengine.

“Hatuna mkurugenzi anayefanya kazi peke yake, wala wakili wa serikali, meneja au mfanyakazi wa ngazi yoyote. Sote ni timu moja yenye wajibu wa kuhakikisha tunafikia malengo ya ofisi kwa pamoja,” amesema Johari.

Aidha, ameeleza kuwa mkutano huo ni fursa muhimu kwa watumishi kubadilishana uzoefu, kujifunza na kuimarisha mshikamano utakaosaidia kuongeza ufanisi wa kazi.

Johari ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya utendaji kazi katika ofisi hiyo ili iendane na mahitaji ya kisasa, huku akiwataka watumishi kuwa tayari kupokea na kuendana na mabadiliko hayo.

“Tunataka kuona ofisi yetu inaakisi taswira ya ufanisi, weledi na uwajibikaji. Lazima tuendane na kasi ya mabadiliko ya kiutendaji ili kuleta matokeo chanya kwa taifa,” alisisitiza.

Ameongeza kuwa maboresho hayo yataongeza uwezo wa ushirikiano kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na taasisi nyingine ndani na nje ya nchi, hatua itakayochochea maendeleo ya sekta ya sheria na kuimarisha utawala bora kwa ujumla.

Mkutano huo wa watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali umewaleta pamoja watumishi kutoka idara mbalimbali kwa lengo la kujadili masuala ya kiutendaji, kuimarisha ushirikiano na kuweka mikakati ya kuboresha huduma kwa umma.







Ends..

Post a Comment

0 Comments