MUSHI ASISITIZA USHIRIKIANO KATIKA MALEZI NA MAKUZI YA MTOTO,SHIRIKA LA GIRL EFFECT LALETA MABADILIKO MAKUBWA KUPITIA MRADI WA UZAZI HODARI

 UZAZI HODARI: WADAU WASISITIZA USHIRIKIANO KATIKA MALEZI NA MAKUZI YA MTOTO

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

KAIMU Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Prosper Mushi, amesema mafanikio ya malezi na makuzi ya mtoto hayawezi kupatikana bila ushirikiano wa sekta mbalimbali, akisisitiza kuwa uwekezaji katika mtoto unapaswa kuanzia akiwa tumboni.

Mushi alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua jukwaa la wadau wa malezi, makuzi na lishe ya mtoto lililofanyika sambamba na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya kijamii, ikiwemo Mradi wa Uzazi Hodari unaotekelezwa na shirika la Girl Effect mkoani Arusha.

Alisema afya, lishe na ustawi wa jamii ni nguzo muhimu katika kujenga msingi imara wa ukuaji wa mtoto, hususan katika kipindi cha ujauzito hadi umri wa miaka miwili, ambacho ni cha maamuzi kwa maendeleo ya baadaye ya mtoto.

“Mama anahitaji lishe bora wakati wa ujauzito na mtoto huduma stahiki baada ya kuzaliwa. Huwezi kuwekeza kwa mtoto bila kuwekeza kwa mama,” alisema Mushi.

Aidha, aliipongeza Serikali kwa kuweka sera na mifumo inayowezesha utekelezaji wa programu za malezi na makuzi, akisema mchango huo umeongeza ufanisi wa huduma kwa jamii.

Hata hivyo, alibainisha kuwepo kwa changamoto za usalama wa watoto, akitoa mfano wa watoto kusafiri na kwenda shule bila tathmini ya kutosha ya usalama, hali inayohitaji ushirikiano wa wazazi, walezi na wadau.

“Afya njema ya mtoto haina maana kama yuko katika mazingira hatarishi. Usalama ni msingi wa kwanza,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Arusha, Denis Mgiye, alisema ofisi yake imekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha Mradi wa Uzazi Hodari unatekelezwa kwa viwango vilivyotarajiwa, hatua inayosaidia kufanikisha malengo ya programu ya taifa.

Mgiye alisema ushirikiano kati ya halmashauri za Arusha DC, Meru na Karatu pamoja na wadau mbalimbali umeimarisha utekelezaji wa mradi huo na kuongeza ufanisi wa huduma za ustawi wa jamii mkoani humo.

“Mafanikio tuliyoyapata katika kipindi cha miaka mitatu ni ya kujivunia na yanapaswa kuendelezwa,” alisema Mgiye.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Girl Effect Tanzania, Dkt. Rita Mbeba, alisema Mradi wa Uzazi Hodari umeleta mabadiliko chanya katika jamii kwa kubadili mitazamo kuhusu malezi, lishe na afya ya mtoto.

Alisema tangu kuanza kwa awamu ya kwanza ya mradi huo mwaka 2023–2024 hadi awamu ya pili inayoendelea hadi Mei 2026, kumekuwa na ongezeko la uelewa na mabadiliko ya tabia katika jamii.

“Tumeona mabadiliko ya kweli katika jamii kuhusu lishe, afya na malezi ya watoto,” alisema.

Dkt. Mbeba alibainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, wadau wa maendeleo na jamii, huku akisisitiza kuwa mbinu za mabadiliko ya tabia zimekuwa na mchango mkubwa.

Aliongeza kuwa mradi huo umeanza katika wilaya za Meru, Karatu na Arusha DC kabla ya kupanuliwa hadi Monduli, ambapo ushiriki wa wananchi na viongozi umeimarika.

Kwa ujumla, wadau hao wamehimiza kuendelea kwa ushirikiano wa sekta mbalimbali, wakisisitiza kuwa uwekezaji katika mtoto ni msingi wa maendeleo ya taifa.






ENDS

Post a Comment

0 Comments