SERIKALI YATAKA UONGOZI MPYA ALAT KUCHOCHEA MAENDELEO YA SERIKALI ZA MITAA KWA USHIRIKIANO NA UADILIFU

 SERIKALI YATAKA UONGOZI MPYA ALAT KUCHOCHEA MAENDELEO YA SERIKALI ZA MITAA KWA USHIRIKIANO NA UADILIFU

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

SERIKALI imetoa wito kwa viongozi wapya wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania kufanya kazi kwa mshikamano, uadilifu na uwajibikaji ili kuimarisha utendaji wa mamlaka za serikali za mitaa na kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Akizungumza jijini Arusha leo Aprili 23, 2026, mara baada ya kukamilika kwa Mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi wa ALAT, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Sospeter Mtwale amesema ushindi wa viongozi hao ni ishara ya imani kubwa waliyopewa na wajumbe, hivyo wanapaswa kuitumia kwa manufaa ya taasisi na wananchi kwa ujumla.

Amesisitiza kuwa uongozi huo mpya una jukumu la kusimamia kwa karibu utekelezaji wa majukumu ya serikali za mitaa, kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi na kuongeza uwazi katika matumizi ya rasilimali za umma.

“Ushindi wenu ni dhamana. Fanyeni kazi kwa ushirikiano, simamieni misingi ya uadilifu na hakikisheni malengo mliyojiwekea yanatekelezwa kwa vitendo,” amesisitiza Mtwale.

Katika uchaguzi huo, Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Constantine Sima, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa ALAT Taifa baada ya kupata kura 273 kati ya kura 339 zilizopigwa, akiwashinda wagombea wenzake kwa tofauti kubwa ya kura.

Katika kinyang’anyiro hicho, Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha alishika nafasi ya pili kwa kura 45, huku Seif Hassan Daud akishika nafasi ya tatu kwa kura 17.

Kwa upande wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Agneta Mpangile aliibuka mshindi baada ya kujizolea kura 189 kati ya kura 337 zilizopigwa. Nafasi ya pili ilichukuliwa na Ali Sadiki Mkaingwa aliyepata kura 118, huku Solomon Mabati akimaliza wa tatu kwa kura 29.

Aidha, zoezi la uchaguzi wa wajumbe wa Kamati Tendaji ya ALAT Taifa limekamilika, huku matokeo yake yakitarajiwa kutangazwa mapema kesho, hatua inayokamilisha rasmi mchakato wa kupata uongozi mpya wa chombo hicho muhimu katika kusimamia maslahi ya serikali za mitaa nchini.

Ends..

Post a Comment

0 Comments