MASHINDANO YA DARTS KUTIKISA JIJI LA ARUSHA KESHO, WACHEZAJI 100+ KUTOKA TANZANIA NA KENYA KUCHUANA VIKALI NI SHAMRASHARA KUELEKEA AFCON

 MCHEZO WA DARTS KUTIKISA JIJI LA ARUSHA KESHO, WACHEZAJI 100+ KUTOKA TANZANIA NA KENYA KUONESHANA KAZI NI SHAMRASHARA KUELEKEA AFCON 

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

Zaidi ya wachezaji 100 wa mchezo wa darts kutoka ndani na nje ya Tanzania wanatarajiwa kushiriki mashindano makubwa yatakayofanyika kesho, Jumamosi Aprili 25, katika Ukumbi wa Bills jijini Arusha.



Afisa Utamaduni na Michezo wa Jiji la Arusha, Benson Maneno, amewakaribisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia mashindano hayo, akieleza kuwa ujio wa washiriki kutoka nchi jirani ya Kenya utaongeza ushindani na hamasa kwa mashabiki.


Amesema mashindano hayo ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha michezo jijini Arusha pamoja na maandalizi ya kuelekea michuano mikubwa ya AFCON 2027, huku yakilenga pia kuifanya Arusha kuwa kitovu cha michezo ya kimataifa.


“Tunawaalika wananchi wote wa Arusha na maeneo ya jirani kufika kwa wingi kushuhudia mashindano haya makubwa ya darts. Ushiriki wa wachezaji kutoka Kenya unaonesha wazi kuwa Arusha inaendelea kupiga hatua katika kukuza michezo,” alisema Maneno.

Kwa upande wake, Mratibu wa mashindano hayo mkoa wa Arusha, Venus Mwanyalo, alisema maandalizi yote yamekamilika na mashindano hayo ni sehemu ya jitihada za kuufufua na kuukuza mchezo wa darts nchini.

“Mashindano haya yanatoa fursa kwa wachezaji wetu kupima uwezo wao dhidi ya wapinzani wa kimataifa, lakini pia kuimarisha ushirikiano wa kimichezo kati ya Tanzania na nchi jirani,” alisema Mwanyalo.

Alibainisha kuwa mashindano hayo yatahusisha michezo ya single, double na chip game, yakianza rasmi saa 3:30 asubuhi na kuendelea hadi Jumapili ambapo bingwa atapatikana.

Kwa mujibu wa Mwanyalo, zawadi za washindi zitatokana na michango ya washiriki, ambapo asilimia 75 ya fedha zitakusanywa zitarudishwa kwa washindi, hatua inayotarajiwa kuongeza ushindani mkubwa.

Aidha, ametoa wito kwa wadhamini kujitokeza kuunga mkono mchezo huo, akieleza kuwa bado unahitaji uwekezaji zaidi ili kufikia viwango vya juu na kuvutia idadi kubwa ya washiriki na mashabiki.

Katika hatua nyingine, Mwanyalo alisema maandalizi ya mashindano ya kimataifa ya Tanzania Open yanaendelea, yatakayofanyika Juni 26 hadi 28 katika ukumbi wa Moshi Club, yakishirikisha nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na Kati.

Mashindano ya kesho yanatarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na ubora na idadi ya washiriki, hali inayoashiria kukua kwa kasi kwa mchezo wa darts na sekta ya michezo kwa ujumla katika jiji la Arusha.







Ends...

Post a Comment

0 Comments