RASILIMALI ASILIA NGUZO YA UCHUMI WA AFRIKA MASHARIKI – DKt. KIJAjI ATOA ONYO KALI DHIDI YA MATUMIZI HOLELA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Waziri wa Maliasili na Utalii, Ashatu Kijaji, amesema mustakabali wa ukuaji wa uchumi wa muda mrefu kwa nchi za Afrika Mashariki unategemea kwa kiwango kikubwa usimamizi madhubuti na endelevu wa rasilimali asilia ikiwemo misitu, wanyamapori na vyanzo vya maji.
Akifungua rasmi mkutano wa 11 wa Mawaziri wa Mazingira wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha Aprili 23, 2026, Dkt. Kijaji alisisitiza kuwa rasilimali hizo si tu urithi wa kizazi cha sasa, bali ni injini muhimu inayochochea ukuaji wa sekta nyeti za uchumi kama utalii, kilimo na nishati.
Alieleza kuwa utajiri wa asili uliopo katika ukanda wa Afrika Mashariki unaipa nafasi ya kipekee katika kuvutia uwekezaji na kuimarisha ustawi wa wananchi, lakini akatahadharisha kuwa bila usimamizi makini, hazina hiyo inaweza kupotea na kuathiri maendeleo ya vizazi vijavyo.
“Hatuwezi kuzungumzia uchumi imara bila kulinda na kusimamia ipasavyo rasilimali zetu asilia. Hizi ndizo msingi wa ajira, kipato cha wananchi na ustawi wa mazingira yetu,” alisisitiza.
Hata hivyo, Waziri Kijaji alionya kuwa rasilimali hizo zinakabiliwa na changamoto kubwa zikiwemo athari za mabadiliko ya tabianchi, ukataji miti holela, ujangili pamoja na matumizi yasiyo endelevu ya ardhi na maji. Alibainisha kuwa hali hiyo inahatarisha sio tu mazingira bali pia maisha ya jamii na uthabiti wa uchumi wa ukanda huo.
Kutokana na changamoto hizo, alizihimiza nchi wanachama wa EAC kuimarisha ushirikiano wa kikanda kwa kuandaa na kutekeleza sera za pamoja zenye mwelekeo wa muda mrefu, pamoja na kuwekeza katika mbinu bunifu za uhifadhi.
Aidha, alitaja masoko ya kaboni kama fursa mpya inayoweza kusaidia nchi za Afrika Mashariki kunufaika kiuchumi huku zikihifadhi mazingira, akisisitiza umuhimu wa kutumia suluhisho zinazotegemea asili (nature-based solutions) katika kupunguza athari za uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kijaji alitoa mwaliko kwa nchi wanachama kushiriki mkutano wa kimataifa wa mazingira ya bahari (COP12) utakaofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Oktoba 2026, akisema mkutano huo utakuwa jukwaa muhimu la kujadili na kuimarisha mikakati ya kulinda ukanda wa pwani na rasilimali za bahari.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umejumuisha mawaziri na viongozi waandamizi kutoka sekta za Muungano, mazingira na maji, ukiwa na dhamira ya kusukuma mbele ajenda ya ukuaji wa uchumi endelevu wa kikanda kupitia uhifadhi wa mazingira.
Kauli ya Waziri Kijaji inaakisi dhamira ya serikali katika kuhakikisha kuwa rasilimali asilia zinalindwa na kutumika kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo, huku ushirikiano wa kikanda ukipewa kipaumbele kama nyenzo muhimu ya kufikia maendeleo jumuishi na endelevu.
Ends..

0 Comments