SIMA ATWAA UENYEKITI ALAT KWA KISHINDO KIKUBWA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Constantine Sima, amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa nchini (ALAT) baada ya kuibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi uliofanyika leo jijini Arusha.
Katika uchaguzi huo uliovutia ushindani mkali, Sima alipata kura 273 kati ya kura halali 338, akimuacha mbali mpinzani wake wa karibu, Meya wa Jiji la Arusha, Maxmillian Ilange, aliyepata kura 45.
Ushindi huo mkubwa unaakisi imani na matarajio makubwa ya viongozi wa serikali za mitaa kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa Sima, ambaye sasa anakabidhiwa jukumu zito la kuongoza na kuratibu shughuli za ALAT katika kipindi kijacho.
Akiwa Mwenyekiti mpya, Sima anatarajiwa kusukuma mbele ajenda za msingi za mamlaka za serikali za mitaa, ikiwemo kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi, kuongeza uwajibikaji, pamoja na kutetea maslahi ya halmashauri mbele ya Serikali Kuu na wadau wa maendeleo.
Jumuiya ya Tawala za Mitaa nchini (ALAT) ni chombo muhimu kinachowakutanisha viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa, kikilenga kuimarisha ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kusukuma mbele agenda za maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika ngazi ya halmashauri.
Uchaguzi huo umefanyika jijini Arusha ukiwa sehemu ya mkutano mkuu maalum wa ALAT, uliowakutanisha viongozi mbalimbali wa serikali za mitaa kutoka pande zote za Tanzania.

0 Comments