DKT. NICAS MAWAZO: NITAIFANYA ALAT KUWA DARUBINI YA MAENDELEO NA SAUTI YA WANANCHI
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
MEYA wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas Mawazo, amesema kuwa yuko tayari kuifanya Jumuiya ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) kuwa chombo imara kitakachotafsiri kwa wananchi mafanikio ya serikali na kusimamia kikamilifu uwasilishaji wa kero zao.
Dkt. Mawazo alitoa kauli hiyo jijini Arusha katika Mkutano Mkuu Maalumu wa uchaguzi ALAT, uliofunguliwa na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Chemba, ambapo pia alitangaza nia yake ya kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa jumuiya hiyo.
Akizungumzia mkutano huo, Dkt. Mawazo aliunga mkono wito wa Waziri Mkuu wa kuwachangia aliyekuwa Mwenyekiti wa ALAT Taifa anayemaliza muda wake, ambaye amepata ulemavu wa kudumu akiwa kazini.
“Nimeguswa na hatua ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na wajumbe wengine. Ni muhimu kuthamini na kuwajali viongozi waliopata madhara wakiwa kazini. Nami nimeamua kuunga mkono kwa kuchangia kile ambacho Mungu amenijaalia,” alisema Dkt. Mawazo.
Akiweka bayana dira yake, alisema ALAT inapaswa kuwa daraja kati ya serikali na wananchi kwa kuhakikisha taarifa za maendeleo zinawafikia wananchi kwa lugha rahisi na inayoeleweka.
“Fedha zinazotolewa na serikali kwenye halmashauri zetu zinajenga madarasa, hospitali na barabara. Wajibu wetu ni kuhakikisha wananchi wanaelewa mchango huo na kuona matokeo yake moja kwa moja,” alieleza.
Aliongeza kuwa chini ya uongozi wake, ALAT itaimarisha zaidi ukusanyaji na uwasilishaji wa kero za wananchi kutoka ngazi za halmashauri hadi serikalini, na kurejesha majibu kwa wananchi kwa uwazi na kwa wakati.
“Sisi ni kiunganishi kati ya wananchi na serikali yao. Tunapaswa kuhakikisha hakuna kero inayopotea njiani, na kila majibu yanayopatikana yanawafikia wananchi,” alisisitiza.
Dkt. Mawazo ameonesha matumaini ya kupata ushindi katika uchaguzi huo, akiahidi kuifanya ALAT kuwa chombo chenye mchango mkubwa katika kusukuma maendeleo ya taifa kupitia serikali za mitaa.
Ends..



0 Comments