SABAYA AKIRI KUKENGEUKA , 'GEREZA LIMENIBADILISHA TABIA NIMEUONA USO WA MUNGU ' ,MBOWE AJITOSA KUMPAKA MAFUTA AOMBA WANA-HAI KUMSAMEHE

 SABAYA AKIRI KUKENGEUKA , GEREZA LIMEMBADILISHA TABIA,AMEUONA USO WA MUNGUGWREZANI MBOWE AMPAKA MAFUTA AOMBA WANA-HAI KUMSAMEHE 

Na Joseph Ngilisho- ARUSHA DIGITAL | HAI 



ALIYEKUWA Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, amesema kupitia kipindi kigumu alichopitia gerezani kumeleta mageuzi makubwa katika maisha yake, akieleza kuwa sasa anaishi kwa kuzingatia maadili, heshima na unyenyekevu katika mahusiano yake ya kila siku.

Sabaya aliyasema hayo wakati akizungumza na wananchi kwenye mazishi yaliyofanyika wilayani Hai, akibainisha kuwa changamoto alizokumbana nazo zilikuwa somo la kipekee lililomjenga upya kiakili na kiroho.

“Nilifanya makosa katika maisha yangu, lakini kupitia yale niliyopitia, nimejifunza kwa namna ambayo sikuitarajia. Kipindi cha gerezani kilinipa nafasi ya kujitafakari na kumtafuta Mungu kwa dhati,” alisema.

Alieleza kuwa tangu kurejea uraiani, kumekuwepo na mabadiliko dhahiri katika mwenendo wake, akisisitiza kuwa sasa anazingatia nidhamu, uvumilivu na mawasiliano yenye heshima kwa watu wote bila kujali tofauti zao.

"Toka nimetoka gerezani mtagundua tembea yangu imebadilika ni ya kikuu, mtagundua ongea yangu sasa ni ya heshima, mtaona kwamba Mungu ameenda kunibadilisha, nimekuwa mtu bora, yaani amekutana na uso qa Mungu amenifanya kuwa chuma chake."- Lengai Ole Sabaya, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai

 Aidha, alibainisha kuwa uzoefu huo umemfundisha umuhimu wa kufanya maamuzi kwa busara na kuepuka papara.

“Leo hii siwezi tena kufanya mambo kwa haraka kama zamani. Nimejifunza kuwa maisha yanahitaji subira, na kila mtu anastahili kuheshimiwa,” aliongeza,

 huku akiwaomba wananchi waendelee kumuunga mkono na kumuombea ili aendelee kuishi kwa misingi ya maadili na uwajibikaji.

Katika tukio hilo hilo, Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, alitoa wito wa msamaha na maridhiano kwa jamii ya Hai, akiwahimiza wananchi kumsamehe Sabaya na kujenga upya mshikamano bila kujali tofauti za kisiasa au kijamii.

Akizungumza Aprili 23, 2026, katika mazishi ya mama wa Mbunge wa Jimbo la Hai (CCM), yaliyofanyika katika Kijiji cha Uduru, Kata ya Machame Kaskazini, Mbowe alisema misiba ni fursa muhimu ya kuwakutanisha watu na kujenga upya mahusiano yaliyoyumba.

“Katika maisha, hakuna binadamu asiye na mapungufu. Tunapaswa kujifunza kusamehe na kujenga upya uhusiano wetu kwa manufaa ya jamii nzima,” alisema Mbowe, akisisitiza umuhimu wa ubinadamu, unyenyekevu na huruma.

Kauli hiyo imekuja katika muktadha wa historia ya kesi zilizomkabili Sabaya mwaka 2021, alipokuwa akikabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka, utakatishaji fedha na rushwa. 

Hata hivyo, Mbowe hakujikita katika tuhuma hizo, bali alihimiza jamii kuangalia mbele na kujenga mshikamano.

Aidha, aliwataka viongozi waliopo madarakani kuendelea kusimamia misingi ya haki, uwajibikaji na utawala bora, akieleza kuwa maendeleo ya taifa yanategemea uongozi unaozingatia sheria na maslahi ya wananchi wote.

Kauli za viongozi hao zimeibua mjadala miongoni mwa wananchi wa Hai, ambapo baadhi wamezipokea kama ishara ya mabadiliko ya kweli na toba ya dhati, huku wengine wakisisitiza kuwa uthibitisho wa mabadiliko hayo utaonekana kupitia vitendo endelevu. 


Hata hivyo, ujumbe wa pamoja wa msamaha, maridhiano na mshikamano umeonekana kugusa hisia za wengi, ukichukuliwa kama hatua muhimu kuelekea kuponya majeraha ya kijamii na kuimarisha umoja.


ENDS..

Post a Comment

0 Comments