DC AFUNGA MAFUNZO YA TARSI ASISITIZA USANIFU BORA WA BARABARA KUDHIBITI AJALI,MHANDISI MASAWE- (TANROADS) ADAI BADO KUNA MATUMZI YASIYOFAA YA BARABARA

 SERIKALI YASISITIZA USANIFU BORA WA BARABARA KUDHIBITI AJALI

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

SERIKALI  imesisitiza umuhimu wa kuimarisha usanifu wa barabara kama njia madhubuti ya kudhibiti ajali na kulinda maisha ya wananchi, ikibainisha kuwa maboresho ya kitaalamu katika miundombinu yameanza kuleta matokeo chanya katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya usalama barabarani jijini Arusha, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Model Mkude, alisema ajali za barabarani zinasababishwa na sababu mbalimbali, lakini usanifu duni wa barabara umeendelea kuwa miongoni mwa changamoto kubwa zinazohitaji ufumbuzi wa haraka.

Alieleza kuwa mafunzo hayo yameweka mkazo katika kuboresha usanifu wa barabara kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu, huku yakitoa mifano halisi ya maeneo yaliyokuwa na ajali nyingi lakini sasa yamepata nafuu baada ya kufanyiwa marekebisho.

“Mfano ni barabara ya Bagamoyo–Tanga ambayo awali ilikuwa nyembamba na yenye kona hatarishi, hali iliyochangia ajali za mara kwa mara. Pia daraja la Mahandelea lilikuwa na changamoto kubwa kabla ya kufanyiwa maboresho,” alisema Mkude.

Aliongeza kuwa baada ya ujenzi wa daraja jipya na kurekebishwa kwa maeneo hatarishi, ajali zimepungua kwa kiasi kikubwa, akitaja pia eneo la Msamvu (Morogoro Plaza) ambapo kona kali iliyokuwa ikisababisha ajali nyingi ilirekebishwa na kuleta nafuu kubwa kwa watumiaji wa barabara.

“Haya ni mafanikio yanayoonesha wazi kuwa tukizingatia taaluma na ushauri wa wataalamu katika usanifu wa barabara, tunaweza kuokoa maisha ya Watanzania wengi,” alisisitiza.

 

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Masawe, alisema pamoja na juhudi za serikali kuboresha miundombinu ya barabara, bado matumizi yasiyo sahihi ya barabara yanaendelea kuhatarisha usalama wa watumiaji.

Alitaja baadhi ya changamoto kuwa ni pamoja na wananchi kufanya biashara pembezoni mwa barabara kuu, hali inayoongeza hatari ya ajali na kuhatarisha maisha.

“Usalama barabarani si jukumu la taasisi moja pekee, bali ni la kila mtumiaji wa barabara kuhakikisha anazingatia sheria na taratibu zilizowekwa,” alisema Masawe.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa wadau katika hatua zote za miradi ya barabara ili kupata maoni ya wananchi na kupanga matumizi sahihi ya maeneo yanayozunguka barabara, hatua inayosaidia kupunguza ajali.

Alionya kuwa ajali za barabarani zina athari kubwa kwa taifa, ikiwa ni pamoja na kupoteza nguvu kazi, kuongezeka kwa gharama za matibabu, uharibifu wa vyombo vya usafiri pamoja na madhara ya kijamii kwa familia za waathirika.

Masawe alibainisha kuwa TANROADS imeanza kuimarisha mchakato wa usanifu kwa kushirikisha wataalamu wa usalama barabarani tangu hatua za awali za miradi, ili kubaini na kurekebisha maeneo hatarishi kabla ya ujenzi kuanza.

“Tunataka kuhakikisha kila mradi wa barabara unazingatia viwango vya usalama tangu usanifu hadi utekelezaji,” aliongeza.

Viongozi hao pia walisisitiza umuhimu wa kuendeleza mafunzo ya usalama barabarani kwa wadau mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari, wapangaji miji, Jeshi la Polisi na wataalamu wa miundombinu, ili kuongeza uelewa mpana wa kudhibiti ajali.

Akihitimisha, Mkude aliwataka washiriki kutumia maarifa waliyojifunza kuboresha utendaji kazi wao, huku Masawe akitoa wito kwa wananchi kushirikiana na serikali kwa kuzingatia sheria za barabarani na kuepuka shughuli hatarishi kandokando ya barabara.

“Ni wakati sasa wa kuchukua hatua kwa pamoja kuhakikisha barabara zetu zinakuwa salama kwa kila mtumiaji,” alisisitiza.






Ends..

Post a Comment

0 Comments