RISASI ZARINDIMA ZAVURUGA IKULU YA MAREKANI,RAIS TRUMP AOKOLEWA KWA KUJIMBIZWA

RISASI ZAVURUGA IKULU: TRUMP AKIMBIZWA GHAFLA, TAIFA LATIKISIKA

By Arushadigital

Rais Donald Trump aliondolewa kwa dharura katika hafla ya kifahari ya White House Correspondents' Dinner iliyokuwa ikifanyika katika Hoteli ya Washington Hilton, baada ya kusikika milio inayodhaniwa kuwa ya risasi na kusababisha taharuki kubwa miongoni mwa wageni waalikwa.

Tukio hilo lililotokea jioni kwa saa za Marekani (sawa na usiku wa kuamkia leo Afrika Mashariki), lilikatiza ghafla hafla hiyo muhimu iliyokuwa imewakutanisha viongozi wakuu wa serikali, wanahabari mashuhuri na watu wenye ushawishi mkubwa nchini humo.

Katika hali ya sintofahamu, maafisa wa usalama waliinua ulinzi wa hali ya juu na kuanza kuwaondoa washiriki mmoja baada ya mwingine, akiwemo Mkurugenzi wa FBI, Kash Patel, huku baadhi ya wageni wakionekana wakikimbia kwa hofu wakitafuta usalama.

Akizungumza baada ya hali kutulia, Trump alifichua kuwa mshambuliaji aliyekuwa na silaha kadhaa alidhibitiwa haraka na maafisa wa Secret Service, akiwapongeza kwa hatua yao ya kishujaa iliyosaidia kuepusha janga kubwa zaidi.

Katika mkasa huo, afisa mmoja wa Secret Service alijeruhiwa kwa kupigwa risasi, lakini alinusurika kifo baada ya kuokolewa na koti maalum la kuzuia risasi. Kwa sasa anaendelea vizuri akiwa chini ya uangalizi wa madaktari.

Taarifa za awali zinaeleza kuwa mshukiwa ni mwanaume mwenye umri wa miaka 31 kutoka California, aliyedaiwa kutekeleza tukio hilo peke yake. Tayari amekamatwa na anatarajiwa kufikishwa mahakamani siku ya Jumatatu.

Picha za kamera za ulinzi (CCTV) zilizochapishwa kupitia mitandao ya kijamii ya Trump zimeanza kusaidia uchunguzi, huku vyombo vya usalama vikichunguza kwa kina chanzo na nia ya shambulio hilo lililotikisa taifa.

Hadi sasa, hakuna vifo vilivyoripotiwa, jambo ambalo linaonekana kuwa faraja pekee katika tukio hilo la kutisha lililoacha maswali mengi bila majibu.

3nds..

Post a Comment

0 Comments