BIASHARA HOLELA YADHIBITIWA SOKO KUU ARUSHA, WAFANYABIASHARA WASEMA HATUA ITAIMARISHA UCHUMI WA MKOA
Na Joseph Ngilisho – Arusha
Wafanyabiashara wa mbogamboga na matunda katika Soko Kuu la Arusha wamempongeza Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, kwa hatua ya kuagiza kuondolewa kwa wafanyabiashara waliokuwa wakifanya biashara nje ya utaratibu rasmi, wakisema hatua hiyo itaimarisha ushindani wa haki, kuongeza mapato ya Jiji la Arusha na kuboresha taswira ya mkoa kama kitovu cha biashara na utalii.
Hatua hiyo imekuja baada ya ziara ya kushtukiza ya mkuu huyo wa wilaya katika soko hilo baada ya kutembelea na kukagua soko hilo na kukumbana na changamoto ya wafanyabishara wa mbogamboga kulalamikiwa na wenzao kupanga bidhaa zao kiholela ikiwemo barabarani na kuacha vizimba vyao walivyopangiwa ndani ya soko hilo na hivyo kuwafanya wafanyabiashara wenye vizimba kukosa wateja.
Hatua hiyo ilitekelezwa jana kupitia zoezi la migambo wa Jiji la Arusha kuwaondoa wafanyabiashara waliokuwa wakipanga bidhaa barabarani na katika maeneo yasiyoruhusiwa ndani na nje ya soko hilo.
Wafanyabiashara walisema biashara holela imekuwa ikisababisha ushindani usio sawa, kupunguza idadi ya wateja kwa wafanyabiashara wanaofuata taratibu na kuathiri mapato ya halmashauri, hali inayodhoofisha mchango wa sekta ndogo ya biashara katika uchumi wa jiji na mkoa kwa ujumla.
Mfanyabiashara wa mbogamboga, Asha Ally, alisema utekelezaji wa utaratibu sahihi wa biashara utasaidia kulinda afya za walaji na kuimarisha hadhi ya Arusha kama jiji linalokua kwa kasi kiuchumi.
“Tunamshukuru Mkuu wa Wilaya kwa hatua hii. Biashara ikifanyika kwa utaratibu inaleta ushindani wa haki, inalinda afya za wananchi na inaongeza mapato ya serikali za mitaa. Hii ni muhimu kwa maendeleo ya Arusha,” alisema Ally.
Aliongeza kuwa bidhaa zinazouzwa katika mazingira yasiyo rasmi mara nyingi huwekwa katika hali isiyo salama kiafya, jambo linaloweza kuhatarisha watumiaji na kuharibu sifa ya soko hilo ambalo linahudumia maelfu ya wakazi wa jiji pamoja na wageni kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.
Kwa upande wake, mfanyabiashara Mwanahamisi Mukunda alisema baadhi ya wafanyabiashara wanaopanga bidhaa kiholela wanamiliki vizimba halali sokoni lakini huwakodisha wengine na wao kuendelea kufanya biashara barabarani kwa faida binafsi.
“Hili linaharibu mfumo wa soko na kuwanyima haki wale wanaofuata sheria. Tunaomba ufuatiliaji uwe wa kudumu ili kulinda utaratibu uliowekwa,” alisema Mukunda.
Wafanyabiashara hao walimuomba Mkuu wa Wilaya pamoja na viongozi wa jiji kufanya ziara za mara kwa mara katika soko hilo ili kuimarisha nidhamu ya biashara na kuzuia kurejea kwa biashara holela.
Kwa mujibu wa wafanyabiashara, udhibiti wa biashara isiyo rasmi utasaidia kuongeza mapato ya Halmashauri ya Jiji la Arusha, kuboresha usafi wa mazingira ya biashara na kuimarisha miundombinu ya masoko, hatua ambazo zina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa mkoa unaotegemea kwa kiasi kikubwa sekta ya huduma, biashara na utalii.
Soko Kuu la Arusha ni miongoni mwa vituo vikuu vya biashara katika ukanda wa Kaskazini, likihudumia wakazi wa jiji pamoja na wafanyabiashara na wageni kutoka mikoa jirani na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hatua ya kudhibiti biashara holela inaelezwa kuwa sehemu ya juhudi pana za mamlaka za mkoa na jiji kuimarisha utawala wa sheria, kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuweka msingi imara wa ukuaji endelevu wa uchumi wa Arusha.
Ends..









0 Comments