AFISA RASILIMALI WATU KIWANDA CHA SUNFLAG ARUSHA AJERUHIWA KWA VISU BAADA YA MGOGORO WA MALIPO KIWANDANI

AFISA RASILIMALI WATU SUNFLAG AJERUHIWA KWA VISU BAADA YA MGOGORO WA MALIPO

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA


Afisa Rasilimali Watu (HR)wa Kiwanda cha Nguo cha Sunflag kilichopo Njiro, jijini Arusha, amejikuta akijeruhiwa vibaya baada ya kushambuliwa kwa visu na mfanyakazi wa kiwanda hicho kufuatia mgogoro wa malipo ya ajira.

Afisa huyo, aliyetambulika kwa jina la Goodluck Mollel, anadaiwa kushambuliwa na mfanyakazi anayejulikana kwa jina moja la Onesmo, ambaye kwa sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi.

Taarifa za awali zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea ndani ya eneo la kiwanda baada ya kutokea kutokuelewana kati ya pande hizo mbili kuhusu madai ya malipo. Inadaiwa kuwa mfanyakazi huyo alitumia kisu kumshambulia Mollel na kumsababishia majeraha katika maeneo ya tumboni, kichwani na mgongoni.

Akizungumza kwa ufupi kutoka nyumbani kwa wazazi wake eneo la Sekei jijini Arusha, Mollel alisema hali yake si nzuri lakini anaendelea na matibabu.

“Naendelea kupata matibabu, lakini bado nahisi maumivu makali… naomba nipumzike,” alisema kwa taabu bila kufafanua zaidi kuhusu tukio hilo.

Hata hivyo taarifa kutoka kiwandani hapo zinadai kwamba Mollel alimwachisha kazi mfanyakazi huyo bila kumlipa stahiki zake na wakati alipofika kiwandani hapo kufuatilia malipo yake kulitokea kutoelewana na kuzuka ugomvi uliopelekea HR kujeruhiwa kwa kisu.

Mkurugenzi wa Kiwanda cha Sunflag, alipotafutwa kutoa ufafanuzi, alisema suala hilo liko mikononi mwa vyombo vya dola na hakuwa tayari kulizungumzia kwa sasa.

Wakati huo huo, jitihada za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, ili kuthibitisha rasmi tukio hilo na kutoa taarifa ya kina zinaendelea.

Tukio hilo limeibua maswali kuhusu usalama mahali pa kazi na utatuzi wa migogoro ya ajira katika viwanda vya uzalishaji jijini Arusha.

Ends..

Post a Comment

0 Comments