PARESO ANG’ARA ARUSHA, ASHUKURU CCM KWA IMANI KUBWA, ASIFIA KWA MAPANA UONGOZI WA RAIS SAMIA

PARESO ANG’ARA ARUSHA, ASHUKURU CCM KWA IMANI KUBWA, ASIFIA KWA MAPANA UONGOZI WA RAIS SAMIA

Ataja mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, asisitiza mshikamano na matumizi ya bima ya afya kwa wote

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Arusha na Mwenyekiti wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Cesilia Pareso, ameendelea kung’ara kisiasa baada ya kutoa shukrani za dhati kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na wabunge wote kwa kumuamini na kumpa dhamana ya kuliongoza Bunge, akiahidi uongozi wa haki, ushirikishwaji na unaozingatia maslahi ya Taifa.


Mh. Pareso aliyasema hayo leo Februari 2,2026 wakati wa hafla ya mapokezi ya Waziri wa Habari, Utamaduni ,Sanaa na Michezo, Paul Christian Makonda, iliyofanyika katika viwanja vya Ngarenaro mkoani Arusha, hafla iliyohudhuriwa na wananchi, viongozi wa Serikali, viongozi wa CCM pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.


Akizungumza mbele ya umati mkubwa huku akishangiliwa, Pareso alimpongeza kwa mapana Rais , Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake thabiti na wenye dira, akieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejipambanua kwa vitendo kupitia utekelezaji wa ahadi zake kwa wananchi, hususan zile alizoahidi kuzitekeleza ndani ya siku mia moja za mwanzo baada ya uchaguzi.


Alisema kuwa chini ya Rais Samia, Serikali imeendelea kusukuma mbele ajenda ya maendeleo kwa kasi kubwa, huku mafanikio yakionekana wazi katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, miundombinu na ustawi wa jamii.


Akitolea mfano sekta ya afya, Pareso alibainisha kuwa ahadi ya Bima ya Afya kwa Wote imeanza kuleta matokeo chanya, ambapo makundi mbalimbali ya wananchi tayari yamenufaika na huduma hiyo muhimu.


“Mpango wa bima ya afya kwa wote ni miongoni mwa mageuzi makubwa yanayoakisi dhamira ya dhati ya Rais Samia ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya bila kikwazo,” alisema Pareso.


Aidha, Mbunge huyo alimpongeza Waziri Makonda, kwa uongozi wake unaojali wananchi na kusimamia vyema majukumu ya Wizara yake, sambamba na kuwapongeza madiwani na wabunge wote wa Mkoa wa Arusha kwa mshikamano wao unaochangia kudumisha amani, utulivu na umoja miongoni mwa wananchi.


Alisisitiza kuwa mshikamano wa viongozi ni nguzo muhimu ya maendeleo, akibainisha kuwa Arusha itaendelea kuwa mfano wa kuigwa kitaifa katika kudumisha amani na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.


Akihitimisha hotuba yake, Mh.Pareso aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kutumia kikamilifu fursa zinazotolewa, hususan kujiunga na mpango wa bima ya afya kwa wote, akisema hatua hiyo itasaidia kuboresha afya za wananchi na kuimarisha maendeleo endelevu ya Taifa.


Ends..


Post a Comment

0 Comments