DKT LUKUMAY AMWAGIA SIFA LUKUKI MAKONDA ASEMA UTEUZI WAKE NI ZAWADI KWA MUNGU,AMWOMBA BARABARA ZA LAMI NA SOKO ARUMERU MAGHARIBI

DKT. LUKUMAY: UTEUZI WA MAKONDA NI CHAGUO LA MUNGU

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA


ARUSHA: Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, amesema kuteuliwa kwa Mbunge wa Arusha Mjini, Paul Makonda, kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ni chaguo la Mungu, akisisitiza kuwa uteuzi huo umezingatia uwezo, uadilifu na dhamira ya kweli ya kulitumikia Taifa.

Dkt. Lukumay alitoa kauli hiyo leo Februali 2,2026 jijini Arusha wakati akizungumza katika hafla ya mapokezi ya Waziri Makonda, iliyofanyika katika viwanja vya Ngarenaro, na kuhudhuriwa na wananchi wengi pamoja na viongozi mbalimbali wakiwemo wabunge, viongozi wa Serikali na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).


Akizungumza mbele ya umati wa wananchi, Dkt. Lukumay alisema uteuzi wa Makonda unaonesha wazi mpango wa Mungu kwa Taifa, akieleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametumika kama chombo cha kuthibitisha mapenzi ya Mungu kwa uongozi wa nchi.

“Si bahati mbaya, si ajali. Huu ni mpango wa Mungu kwa Taifa letu. Kuteuliwa kwa Paul Makonda ni chaguo la Mungu kwa wakati huu,” alisema Dkt. Lukumay.

Katika hatua nyingine, Dkt. Lukumay alimwomba Waziri Makonda kutumia nafasi yake kusaidia kusukuma maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Jimbo la Arumeru Magharibi, hususan katika sekta ya miundombinu na utalii, akibainisha kuwa miradi hiyo itaongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi na mapato ya Serikali.

Kwa mujibu wa Dkt. Lukumay, aliiomba Serikali kupitia wizara husika kuharakisha ujenzi wa barabara ya Sambasha hadi Ngaramtoni, akieleza kuwa barabara hiyo itarahisisha upatikanaji wa vivutio vya utalii, hususan wanyama adimu aina ya Mbega (Black and White Colobus Monkeys) wanaopatikana Mlima Meru pekee, hivyo kuongeza mvuto wa utalii katika eneo hilo.

Aidha, aliomba ujenzi wa barabara ya lami kutoka Sekei hadi Olgilai, pamoja na barabara ya Mbauda – Oljoro – Losunyai, akisema miundombinu hiyo ni muhimu kwa wananchi wanaojishughulisha na kilimo na biashara, kwani itawawezesha kusafirisha mazao yao kwa urahisi kwenda masokoni na hivyo kuongeza kipato chao.

Vilevile, Dkt. Lukumay alisisitiza umuhimu wa kujengwa kwa soko la kisasa Ngaramtoni, akieleza kuwa mradi huo utaongeza fursa za biashara, kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kuboresha maisha ya wananchi wa Arumeru Magharibi kwa ujumla.

Alihitimisha kwa kuwataka wananchi wa Arusha kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na amani, akisema maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana bila ushirikiano wa viongozi na wananchi kwa pamoja.

Kwa upande wake, Waziri Makonda aliwashukuru wananchi wa Arusha kwa mapokezi makubwa, akiahidi kushirikiana na viongozi wote kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wa maeneo yote ya Mkoa wa Arusha.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kikanda, ikionesha mshikamano mkubwa wa kisiasa na kijamii miongoni mwa viongozi na wananchi wa Mkoa wa Arusha.



Ends..

Post a Comment

0 Comments