WABUNGE ARUSHA WAWAHIMIZA WANANCHI KUMPA IMANI MAKONDA
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
MBUNGE wa Jimbo la Monduli na Katibu wa Wabunge wa Mkoa wa Arusha, Isack Joseph, amewataka wananchi wa Mkoa wa Arusha kuitambua, kuilinda na kuitumia kikamilifu fursa ya maendeleo iliyokuja na uongozi wa Mbunge wa Arusha Mjini na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Christian Makonda, kufuatia uteuzi wake katika wadhifa huo wa kitaifa.
Isack aliyasema hayo Februari 3, 2026, wakati akizungumza katika hafla ya mapokezi rasmi ya Waziri Makonda, yaliyoandaliwa baada ya kuteuliwa kwake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kufanyika katika Viwanja vya Ngarenaro, Jijini Arusha.
Akizungumza mbele ya mamia ya wananchi, Mh.Isack alisema uteuzi wake kama Katibu wa Wabunge wa Mkoa wa Arusha ulitokana na heshima na imani waliyopewa na wabunge wenzao wa ukanda huu, akisisitiza kuwa nafasi hiyo ni dhamana ya kuwatumikia wananchi kwa uaminifu na uwajibikaji.
“Leo nilitamani kutumia fursa hii kuzungumza na Watanzania, hususan wana Arusha, kuwaomba kwa unyenyekevu mkubwa—Makonda amekuja kutubadilisha maisha. Narudia tena, Makonda amekuja kutubadilisha maisha,” alisema Mh. Isack huku umati wa wananchi ukimshangilia.
Alieleza kuwa ujio wa Waziri Makonda, mara baada ya uteuzi wake, umefungua ukurasa mpya wa matumaini na fursa za kiuchumi, kijamii na kimaendeleo kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha.
“Makonda amekuja na dhamira ya kutuunganisha na kutujengea mazingira bora ya fursa—fursa za ajira, biashara na maendeleo kwa ujumla. Tusiitupe fursa hii. Kuna watakaosema mengi, lakini ukweli unabaki—Makonda ni mtu muhimu kwetu na kwa mustakabali wa Arusha,” alisisitiza.
Mh.Isack pia alirejea historia ya uongozi wa Waziri Makonda, akieleza kuwa ni kiongozi aliyedhihirisha uwezo mkubwa katika ngazi mbalimbali za serikali, hali iliyomfanya kuaminiwa na kupewa nyadhifa nzito.
“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alimwona Makonda, akamteua kuwa Naibu Waziri, akaendelea kumuamini akamteua kuwa Waziri. Na leo, mara baada ya uteuzi huo, amewasili Arusha kwa dhamira ya kuwatumikia wananchi na kuwasukuma mbele kimaendeleo,” alisema.
Katika hitimisho lake, Mheshimiwa Isack aliwataka wananchi wa Arusha kumpa Makonda imani, ushirikiano na sapoti ya dhati ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
“Mkopesheni imani, mpeni imani, mshirikianeni naye. Tukifanya hivyo, Mkoa wa Arusha utapiga hatua kubwa za maendeleo,” alisisitiza.
Hafla hiyo ya mapokezi, iliyofanyika mara baada ya uteuzi wa Waziri Makonda, ilihudhuriwa na wabunge mbalimbali wa Mkoa wa Arusha na ukanda wa Kaskazini, pamoja na viongozi wa serikali, kimila, kisiasa, na wananchi kutoka maeneo mbalimbali, ikionesha mshikamano na matumaini mapya ya maendeleo kwa Mkoa wa Arusha.
"Tupeni imani sisi wabunge wa Arusha tupo 11 tutashirikiana na Makonda tutashirikiana na Rais Samia kuujenga Mkoa wa Arusha ,niwaombe sana najua kuna mambo mnataka tukayatekeleze tupeni imani sisi ni kitu kimoja hata wanaMonduli najua changamoto inayowasumbua"
"Nataka niwaambie,nitakwenda kuwasemea Bungeni nataka niwaambie mmetuma jembe sijaenda bungeni kulala nimekwenda kuwasemea watanzania na hata wana Monduli hata leo bungeni swali langu la msingi niliuliza ni lini serikali itapeleka fedha za kutosha kuhakikisha watu wa Monduli wanapata maji"Alisema
Ends..


0 Comments