WAFANYAKAZI ZAIDI YA 200 WA KIWANDA CHA NONDO CHA BANSAL STEEL ARUSHA WAMEGOMA , WAKATAA KUPUNGUZIWA MISHAHARA

 WAFANYAKAZI ZAIDI YA 200 WA KIWANDA CHA NONDO CHA BANSAL STEEL ARUSHA WAMEGOMA , WAKATAA KUPUNGUZIWA MISHAHARA

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

Zaidi ya wafanyakazi 200 wa kiwanda cha kutengeneza nondo cha Bansal Steel Rolling Ltd, kilichopo eneo la Kisongo jijini Arusha, wamegoma kufanya kazi wakipinga kile walichodai ni mpango wa mwajiri wao kupunguza mishahara yao na kuwalipa kima cha chini cha serikali cha Sh 200,000.


Wakizungumza nje ya lango la kiwanda hicho, wafanyakazi hao walisema walipokea taarifa za kupunguziwa mishahara kutoka kiwango walichokuwa wakilipwa awali kati ya Sh 216,000 hadi Sh 252,000 na badala yake kulipwa kima cha chini cha serikali kwa sekta ya viwanda, jambo walilodai halikubaliki kutokana na ugumu wa maisha unaoendelea.


Walieleza kuwa nyongeza ya mishahara iliyotangazwa na serikali ililenga kuwasaidia wafanyakazi kukabiliana na gharama za maisha, hivyo walishangazwa na uamuzi wa mwajiri wao kuwapunguzia mishahara ilhali awali walikuwa wakilipwa zaidi ya kima cha chini cha serikali

Mbali na hilo, wafanyakazi hao walidai kutolipwa ipasavyo malipo ya muda wa ziada (overtime), huku wakiiomba serikali kupitia Wizara ya Kazi kuingilia kati na kutoa ufafanuzi wa kisheria kuhusu mishahara na stahiki zao kwa sasa.


Aidha, walibainisha changamoto ya ukosefu wa vitendea kazi muhimu ikiwemo viatu vigumu na kofia ngumu, wakisisitiza kuwa kazi wanayofanya ni hatarishi kutokana na joto kali na moto unaotokana na kuyeyusha vyuma. Kwa mujibu wao, mazingira hayo yanaweka maisha yao hatarini kila siku.


Katika hatua nyingine, wafanyakazi hao waliituhumu Idara ya Kazi mkoani Arusha kwa kile walichodai ni kushindwa kuwasikiliza na kuchukua hatua stahiki dhidi ya malalamiko yao, wakidai maofisa wake hufika kwenye ofisi za waajiri na kuondoka bila kutoa suluhu.


Akijibu madai hayo, meneja wa kiwanda cha Bansal Steel Rolling Ltd alisema anashangazwa na hatua ya wafanyakazi wake kugoma, akieleza kuwa mshahara wanaolipwa unazidi kiwango cha kima cha chini cha serikali.


Alifafanua kuwa kwa sasa kiwanda hicho hulipa hadi Sh 420,000 kwa kujumlisha na malipo ya muda wa ziada, akidai malipo hayo hutolewa bila kujali kama mfanyakazi ameingia kazini au la. 


Meneja huyo alisisitiza kuwa hajawahi kuandika wala kutoa barua yoyote ya kupunguza mishahara ya wafanyakazi hao, na kwamba hafahamu walipopata taarifa hizo.


Mwisho, aliwaomba wafanyakazi kurejea kazini huku uongozi wa kiwanda ukiendelea kushughulikia madai yao kwa njia ya mazungumzo, ili kuepusha athari kwa uzalishaji na ustawi wa pande zote mbili.


Ends..

Post a Comment

0 Comments