MARTHA GIDO AMSHUKURU RAIS SAMIA KWA UTEUZI WA MAKONDA, WABUNGE ARUSHA WAJIPANGA KUSUKUMA MAENDELEO KWA UMOJA

MARTHA GIDO AMSHUKURU RAIS SAMIA KWA UTEUZI WA MAKONDA, WABUNGE ARUSHA WAJIPANGA KUSUKUMA MAENDELEO KWA UMOJA

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

ARUSHA: Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Arusha kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mh.Martha Gido, amemshukuru Rais  Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumuamini na kumteua Mh.Paul Makonda kuwa Mbunge wa Arusha na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, akieleza kuwa uteuzi huo umefungua ukurasa mpya wa kasi ya maendeleo katika Mkoa wa Arusha.



Akizungumza februali 2,2026 wakati wa mkutano mkubwa wa mapokezi ya Mh.Makonda uliofanyika katika Viwanja vya Ngarenaro, jijini Arusha, Mh. Gido alisema uamuzi wa Rais Samia unaonesha dhamira ya dhati ya serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha uongozi wenye maamuzi, uwajibikaji na matokeo chanya kwa wananchi.

“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maamuzi yake yenye tija. Uteuzi wa Mheshimiwa Makonda ni ishara ya imani kubwa ya Rais kwa Mkoa wa Arusha na uthibitisho kuwa serikali imedhamiria kuusukuma mkoa huu mbele kimaendeleo,” alisema Gido.

Gido alisisitiza kuwa wabunge wote wa Mkoa wa Arusha wamejipanga kufanya kazi kwa umoja na mshikamano, wakizungumza lugha moja katika kumsaidia Rais na kushirikiana kwa karibu na Waziri Makonda ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa kasi na ufanisi mkubwa.

Alibainisha kuwa maslahi ya wananchi ndiyo yatakuwa kipaumbele kikuu, huku akieleza kuwa tofauti za kisiasa hazitapewa nafasi mbele ya agenda ya maendeleo ya Arusha.

“Sisi kama wabunge wa Arusha tumeamua kusimama pamoja. Tutafanya kazi kwa umoja, tutazungumza lugha moja na tutahakikisha Arusha inanufaika kikamilifu na fursa za maendeleo zinazotolewa na serikali,” aliongeza.

Aidha, alisema ujio wa Mheshimiwa Makonda umeongeza matumaini mapya kwa wananchi kutokana na uzoefu wake wa kiuongozi, kasi ya utendaji na uwezo wa kusimamia maelekezo ya serikali kwa vitendo.

Mkutano wa mapokezi hayo ulipambwa na mahudhurio ya mamia ya wananchi, viongozi wa chama na serikali, viongozi wa mila na wazee wa kimila, hali iliyoonesha mshikamano mkubwa wa kijamii na kisiasa ndani ya Mkoa wa Arusha.

Baada ya hotuba za viongozi mbalimbali, tukio hilo lilihitimishwa kwa wananchi na viongozi kuburudika pamoja katika mazingira ya amani na umoja, wakishiriki burudani ya nyama choma, jambo lililoakisi ukaribu wa viongozi na wananchi pamoja na kuimarika kwa mahusiano ya kijamii katika mkoa huo.

Ends..

Post a Comment

0 Comments