MAKONDA ATOA ONYO KALI KWA VIONGOZI WANAOCHOCHEA MIGOGORO YA MAENDELEO ARUSHA
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
Mbunge wa Arusha na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Paulo Makonda, ametoa onyo kali kwa viongozi wanaoendeleza malumbano, migogoro ya kijamii na kisiasa isiyo na tija, akisema tabia hiyo inarudisha nyuma juhudi za maendeleo na haitavumiliwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Makonda alitoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya mradi wa Soko la Kilombero jijini Arusha, ambapo alisisitiza kuwa serikali na chama tawala vimejipanga kuhakikisha miradi ya maendeleo inaleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi, bila kukwamishwa na maslahi binafsi ya baadhi ya viongozi.
Alisema kuna baadhi ya viongozi wanaojitokeza kuchochea migogoro isiyo na msingi, badala ya kushirikiana katika kusukuma mbele ajenda ya maendeleo, jambo ambalo linawanyima wananchi fursa za kiuchumi zinazotokana na miradi mikubwa kama masoko, stendi na miundombinu mingine.
"Nitumie fursa hii kumwomba mstahiki Meya pamoja na Naibu Meya shikamaneni ,sisi muda mwingi tunaweza tusiwepo ,mkianza migogoro nyinyi mnabahati mbaya sana mbunge wenu ni MNEC nitawashughulikia kupitia nafasi yangu ya UNEC tusirudi tulipotoka"
“CCM haiwezi kuwa chama cha migogoro na malumbano. Tunataka viongozi wanaojenga, wanaosimamia maendeleo na kuwatumikia wananchi. Yeyote atakayeendelea kuchochea migogoro isiyo na tija, nitamshughulikia ndani ya chama,” alisema Makonda kwa msisitizo.
Makonda aliongeza kuwa kwa nafasi yake ya sasa kama Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, ana wajibu wa kuhakikisha nidhamu, mshikamano na maadili ya uongozi yanaimarishwa, hasa katika maeneo yanayotekeleza miradi mikubwa ya kimkakati.
Akizungumzia mradi wa Soko la Kilombero, Makonda alieleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa, akibainisha kuwa soko hilo litakuwa kichocheo kikubwa cha uchumi wa wananchi, wafanyabiashara wadogo na wakubwa, pamoja na ajira kwa vijana wa jijini Arusha.
Aliwataka viongozi wa serikali za mitaa, watendaji na wanachama wa CCM kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa, huku maslahi ya wananchi yakipewa kipaumbele cha kwanza.
Kauli hiyo ya Makonda imepokelewa kwa hisia tofauti, huku wananchi na wadau wa maendeleo wakieleza matumaini kuwa msimamo huo utasaidia kupunguza migogoro isiyo ya lazima na kuimarisha kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Arusha.
Ends







0 Comments