UWT ARUSHA MJINI YAMPONGEZA RAIS SAMIA KWA USHINDI NA KUIINUA ARUSHA KITAIFA
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
ARUSHA — Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Arusha Mjini, Mary Kisaka, ameongoza baraza la kawaida la wilaya hiyo kutoa pongezi za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ushindi mkubwa alioupata katika uchaguzi pamoja na uongozi wake thabiti unaoendelea kuilinda amani ya nchi.
Akizungumza leo januari 14,2026 wakati wa baraza hilo Makao Makuu ya CCM Mkoa, Kisaka alisema kikao hicho kimefanyika katika mazingira ya amani na utulivu, hali iliyowezeshwa na baraka za Mwenyezi Mungu, na kujadili agenda mbalimbali za maendeleo na masuala ya kijamii yanayowahusu wananchi wa Arusha Mjini.
“Moja ya agenda muhimu tulizojadili ni kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushindi mkubwa alioupata katika uchaguzi, ushindi unaoonesha imani kubwa ya wananchi kwake, hususan wanawake waliompa kura kwa zaidi ya asilimia 93,” alisema Kisaka.
Alieleza kuwa ushindi huo ni wa kihistoria na ni fahari kwa taifa, hasa kwa wanawake wa Tanzania, akisisitiza kuwa umeonesha nafasi na mchango mkubwa wa mwanamke katika uongozi na maendeleo ya nchi.
Katika hatua nyingine, baraza hilo pia limempongeza Rais Samia kwa uamuzi wa kumteua Mbunge wa Jimbo hilo, Mheshimiwa Christian Makonda, kuwa Naibu Waziri, hatua ambayo imeonesha imani kubwa ya Rais kwa viongozi wa Arusha.
Kadhalika, Kisaka alisema UWT Arusha Mjini inamshukuru Rais kwa uteuzi wa Waziri wa Habari na Michezo kutoka Arusha, akibainisha kuwa ni tukio la kihistoria kwa jiji hilo ambalo kwa takribani miaka 115 halijawahi kupata Waziri kutoka eneo hilo.
“Huu ni uthibitisho wa wazi kuwa Rais ameiona Arusha, ameithamini na ameiamini,” alisisitiza.
Akizungumzia suala la amani, Kisaka alimpongeza Rais Samia kwa uongozi wake makini katika kipindi kigumu baada ya uchaguzi, akisema alisimama imara kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani, utulivu na mshikamano.
“Kwa busara, uvumilivu na hekima yake, changamoto mbalimbali zilitafutiwa ufumbuzi na taifa likaendelea kuwa salama. Bila uongozi wake thabiti, amani hii isingeweza kudumu,” alisema.
Aliongeza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo, akisisitiza kuwa katika mazingira ya amani, wananchi hufanya kazi kwa bidii, familia huishi kwa utulivu na watoto hukulia katika mazingira salama.
Kisaka pia alibainisha nafasi ya mwanamke katika kulinda na kudumisha amani, akisema amani ya jamii huanzia nyumbani, na mwanamke ana jukumu kubwa la kulea kizazi chenye maadili na uzalendo.
Aidha, aliwataka vijana kuendelea kuwa walinzi wa amani ya taifa, akisema wao ni nguvu kazi na nguzo muhimu ya mshikamano wa jamii na maendeleo ya nchi.
“Tunawahimiza vijana wetu kuwa watulivu, wavumilivu na wazalendo ili Tanzania iendelee kubaki kuwa kisiwa cha amani barani Afrika,” alisema.
Kwa ujumla, baraza la UWT Wilaya ya Arusha Mjini limeendelea kumpongeza na kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake mahiri, kwa kuimarisha amani, kwa kuilinda Arusha na kwa maamuzi yenye maslahi mapana kwa taifa, huku likimuombea afya njema na mafanikio mema katika kuiongoza nchi.
Amani ni tunu ya taifa, na kila Mtanzania ana wajibu wa kuilinda.
Ends







0 Comments