MKUU WA WILAYA ARUSHA ATOA SIKU TATU KWA MACHINGA KUONDOKA BARABARANI
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
ARUSHA January 14,2016—Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, amewapa siku tatu wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga wanaofanya biashara pembezoni mwa barabara na mbele ya maduka ya wafanyabiashara halali kuondoka mara moja na kurejea katika vizimba na maeneo maalum waliyopangiwa na Serikali.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya wafanyabiashara wa maduka jijini Arusha kutishia kuitisha mgomo usio na kikomo wa kufunga maduka yao, wakilalamikia uvamizi wa machinga wanaopanga bidhaa mbele ya maduka yao, hali wanayodai inahatarisha uwekezaji wao na kupunguza mapato huku wakiendelea kulipa kodi na tozo mbalimbali kwa Serikali.
Akizungumza na wafanyabiashara pamoja na viongozi wa masoko jijini Arusha, Mkude alisema Serikali tayari imefanya uwekezaji mkubwa katika kuandaa miundombinu rafiki kwa wafanyabiashara wadogo, ikiwemo ujenzi wa vibanda, vizimba na masoko maalum yaliyoainishwa kisheria.
“Serikali imejenga na kuandaa maeneo maalum ya biashara kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo ili wafanye shughuli zao kwa utaratibu, usalama na kwa kuzingatia sheria. Hakuna sababu ya kuendelea kufanya biashara barabarani au mbele ya maduka ya watu wengine,” alisema Mkude.
Alifafanua kuwa maeneo yanayotumiwa na wafanyabiashara walioko madukani ni halali na yana mifumo rasmi ya uendeshaji pamoja na uongozi unaotambulika, hivyo hayapaswi kuvamiwa na wafanyabiashara wasio rasmi.
Mkude alionya kuwa biashara zinazofanywa barabarani na katika maeneo yasiyotambuliwa kisheria husababisha usumbufu wa mazingira ya mji, migongano isiyo ya lazima baina ya wafanyabiashara, pamoja na hatari za kiusalama kwa watumiaji wa barabara.
“Hali hii pia inawaumiza wafanyabiashara waliowekeza kwa kufuata taratibu zote, kwa sababu inawanyang’anya wateja na kuvuruga ushindani wa haki katika biashara,” aliongeza.
Mkuu huyo wa Wilaya alisisitiza kuwa baada ya siku tatu hakuna atakayevumiliwa kuendelea kufanya biashara nje ya maeneo yaliyopangwa, akibainisha kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekaidi agizo hilo.
Aidha, aliwataka wadau wote wa biashara kushirikiana na mamlaka za Serikali kwa lengo la kulinda ustawi wa jiji la Arusha, kudumisha amani ya kibiashara na kuchochea maendeleo ya uchumi ~kwa~ manufaa ya wananchi wote
Wakizungumza na vyombo vya habari jijini hapa jana, viongozi wa jumuiya ya wafanyabiashara wamesema hali hiyo imekuwa ikishamiri kwa muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi wa kudumu, licha ya wao kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi na tozo mbalimbali serikalini.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Arusha, Loken Adolf, alisema zaidi ya maduka 14,000 katika mitaa mbalimbali ya jiji hilo yameathirika moja kwa moja na uwepo wa machinga wanaofanya biashara kiholela mbele ya maduka yao.
Alisema jumuiya hiyo imekuwa ikifanya vikao vingi na viongozi wa serikali za mitaa na wilaya kuhusu kadhia hiyo, lakini hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa hadi sasa, jambo linalowaacha wafanyabiashara wakiumia huku wakibebeshwa mzigo mkubwa wa kodi.
“Kumekuwa na taarifa zinazodai kuwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, amewaruhusu mamachinga kupanga bidhaa zao popote. Sisi tunasema taarifa hizo si za kweli, na tunaomba Serikali ya Mkoa itoe ufafanuzi wa wazi kwa sababu hali hii inatuumiza sana wafanyabiashara wanaolipa kodi,” alisema Adolf.
Aliongeza kuwa tangu Agosti mwaka jana, wafanyabiashara wamekuwa wakikabiliwa na usumbufu mkubwa kutoka kwa mamachinga wanaowazunguka na kupora wateja wao, hali iliyosababisha baadhi ya maduka kushindwa kujiendesha kibiashara.
“Tumevumilia kwa muda mrefu, sasa imefika mwisho. Tuko tayari kufunga maduka yetu na kuacha kulipa kodi iwapo hatutapata suluhisho. Hatuwezi kuendelea kulipa kodi wakati hatuzalishi chochote,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wilaya ya Arusha, Dominick Mollel, alimtaka Mkurugenzi wa Jiji la Arusha kuchukua hatua za haraka na kutoingiza siasa katika suala hilo, akisema wamachinga wamekuwa wakipanga bidhaa zao katikati ya barabara na mbele ya maduka, hali inayochangia msongamano na hatari kwa usalama.
Mollel alisema endapo tatizo hilo halitapatiwa ufumbuzi wa haraka, wafanyabiashara hawatasita kufunga maduka yao hadi Serikali itakapochukua hatua stahiki.
Wafanyabiashara hao walisisitiza kuwa hawapingi uwepo wa machinga, bali wanahitaji kuwepo kwa utaratibu rasmi, usawa wa kisheria na haki ya walipakodi, ili kuhakikisha shughuli za biashara zinafanyika kwa manufaa ya pande zote na kwa ustawi wa uchumi wa jiji la Arusha.
Ends..





0 Comments